Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema kuna njama ya kumtia mbaroni Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya huko The Hague wakati kesi yake itakapoanza katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC Julai 9.
Museveni ameyadokeza hayo mjini Addis Ababa Ethiopia wakati akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya IGAD ya Pembe na Mashariki mwa Afrika.
Katika hotuba yake ya Ijumaa usiku, Museveni alisema ICC haina nia njema katika kesi inayowahusu Wakenya watatu ambao ni rais Kenyatta, naibu wake William Ruto na mwandishi habari Joshua Sang.
Museveni amenukuliwa akisema kuwa viongozi wa IGAD hawataafiki Kenyatta kuhudhuria kesi ya ICC iwapo nia ni kumtia mbaroni. Ameonya kuwa iwapo ICC haitaweka wazi nia yake, basi uhusiano wa ICC na Afrika utazorota. Amesema mahakama hiyo ya kimataifa inapaswa kuwaheshimu viongozi wa Afrika. Rais Museveni anaongoza mkakati wa viongozi wa Umoja wa Afrika wanaotaka ICC itupilie mbali kesi dhidi ya Kenyatta. Imearifiwa kuwa nchi zote za Afrika isipokuwa Botswana zimeunga mkono mtazamo wa Museveni. Hali kadhalika mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Bi. Nkosazana Dlamini Zuma amenukuliwa akisema matatizo ya Afrika yanapaswa kutatuliwa na Waafrika wenyewe.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO