Monday, May 20, 2013

NETANYAHU ATISHIA KUISHAMBULIA TENA SYRIA

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni ametishia kuwa utawala huo utatekeleza shambulizi jingine la anga dhidi ya Syria. Netanyahu aliyasema hayo hapo jana na kuongeza kuwa, katika kulinda maslahi yake Israel imeazimia kutekeleza shambulizi jingine la anga dhidi ya Syria. Aidha waziri mkuu huyo wa utawala bandia wa Kizayuni, amesisitiza kuwa, Israel haitofumbia macho chaguo lolote kuhusu serikali ya Syria. Hivi karibuni ndege za utawala huo, zilitekeleza shambulizi la anga dhidi ya kituo cha utafiti cha Jamaraya katika viunga vya mji mkuu Damascus na kupelekea watu kadhaa kuuawa. Aidha mnamo Januari mwaka huu ndege za Israel zilitekeleza shambulizi jingine dhidi ya kituo hicho. Wakati huo huo duru za habari nchini Syria zinaarifu kuwa, jeshi la nchi hiyo limepiga hatua kubwa katika mapambano yake na magaidi katikati ya mji wa al-Qusair uliopo karibu na mpaka wa Lebanon. Habari zaidi zinasema kuwa, mapigano kati ya jeshi na waasi katika eneo hilo, bado yanaendelea na kwamba, hadi sasa zaidi ya waasi 70 wameuawa na makumi ya wengine kujisalimisha kwa jeshi la Syria.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO