Sunday, May 12, 2013

UTATA WAIBUKA KENYA BAADA YA KUANDIKWA BARUA KUFUTA KESI YA ICC


Serikali ya Awamu ya Nne nchini Kenya imeendelea kuandamwa na mzimu wa kesi ya inayowakabili Rais Uhuru Muigai Kenyatta na Naibu wake William Samoei Arap Ruto ambao sasa wanataka kesi dhidi yao itupiliwe mbali. Serikali ya Nairobi imeandika barua kwenda kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC kuliomba kufuta kesi hiyo iliyopo mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC wakikabilia na makosa ya kuchochea mauaji.
Balozi wa Kenya katika Umoja Mataifa UN Macharia Kamau ndiye aliandika barua hiyo akitaka kufungwa kwa mashtaka hayo ya uhalifu wa kibinadamu yanayowakabili Viongozi hao wajuu wa Serikali hiyo. Barua hiyo inaweka wazi kabisa ombi la Kenya kwa Baraza la Usalama ni kutaka kufutwa kabisa kwa kesi hizo ambazo zinawakabili Viongozi hao wanaotajwa kuchochea mauaji yaliyofanyika baada ya kuzuka kwa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/2008.
Serikali ya Kenya iliandika barua hiyo tarehe pili ya mwezi May na kugongwa mhuri wa siri na inakuwa ombi la kwanza rasmi kutoka Nairobi kutaka kufutwa kwa kesi hiyo iliyozua tofauti ya kimsimamo. Hakuna majibu yoyote ambayo yametolewa na Baraza la Usalama tangu kuwasilishwa kwa barua hiyo ya kutaka kufutwa kwa mashtaka yanayowakabili Viongozi wa juu wa Serikali ya Awamu ya Nne. Kwa upande wake Naibu Rais Ruto amekataa kuhusika kwenye mpango huo wa kutaka kufutwa kwa kesi hiyo iliyopo ICC na badala yake amesema anaiheshimu Mahakama hiyo kama chombo huru.
Wakili wa Naibu Rais Ruto, Karim Khan amesema mteja wake anaridhika na namna ambavyo kesi hiyo inavyendelea na ana imani kubwa Mahakama ya ICC itatoa haki kwa kufuata sheria. Rais Kenyatta, Naibu Rais Ruto na Mwandishi wa Habari Joshua Arap Sang wanatuhumiwa kwa kuchochea na kufadhili machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/2008 na kusababisha zaidi ya watu 1000 kupoteza maisha.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO