Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya nchini Lebanon Hizbullah, ameashiria vitisho vinavyowakabili wananchi wa Palestina na kusisitiza kuwa, misimamo ya watawala wa nchi za Kiarabu kuhusiana na suala hilo ni ya kufedhehesha. Sayyid Nasrullah amesema kuwa, watawala wa nchi za Kiarabu wanaamiliana na maudhui ya wakimbizi wa Kipalestina, Masjidul Aqswa, Baitul Muqaddas na makanisa ya kale katika eneo hilo kama tatizo dogo la kihistoria na wala sio kama lengo tukufu la Wapalestina. Amesema kuwa, watawala wa Kiarabu wamekuwa na misimamo ya kindumakuwili na ya kimaslahi kuhusu kadhia ya Palestina na kuwa hawaitambui kuwa ni ya Kiislamu. Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kuwa, kuendelezwa vitendo vya ukandamizaji vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi eneo la Quds Tukufu, kutiwa mbaroni Mufti wa Quds na kuingia walowezi wa Kizayuni katika Msikiti wa al Aqswa, limekuwa jambo la kawaida kwa Wazayuni hao. Hata hivyo Sayyid Nasrullah amesema kuwa, wananchi shujaa wa Palestina wameweza kukabiliana na matatizo hayo makubwa, bila ya kupata uungaji mkono wa kutosha kutoka kwa mataifa ya Kiislamu na Kiarabu. Miongoni mwa jinai zinazofanywa na Wazayuni ni kuchimbwa njia na mashimo chini ya Masjidul Aqsa, kubomolewa nyumba za Wapalestina mashariki mwa Baitul Muqaddas na kuwaondoa kwa nguvu kwenye makazi yao ya asili. Sayyid Nasrullah amezikosoa vikali nchi za Kiarabu kuhusiana na mgogoro ulioko baina ya Palestina na Israel na kusema kuwa, inaonekana wazi kwamba watawala wa Kiarabu wako tayari kuupendelea utawala wa Israel kuliko ndugu zao wa Kipalestina. Amesema, zamani ilikuwa ikidaiwa kuwa, kama lingetupwa jiwe moja tu kwenye Masjidul Aqswa, ulimwengu wa Kiarabu ungelitoa radiamali kali, amma jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, leo hii baadhi ya mataifa ya Kiarabu na hata viongozi wa harakati za Kiislamu wanakariri kwenye hotuba zao matamshi yaleyale yaliyotamkwa na Bill Clinton Rais wa zamani wa Marekani, mara baada ya kufanyika mazungumzo kati Yasser Arafat kiongozi wa zamani wa PLO na Ehud Barak Waziri Mkuu wa zamani wa Israel. Kiongozi wa Hizbullah amesema kuwa, inasikitisha kuona kuwa, baadhi ya wakuu wa nchi za Kiarabu badala ya kulipa kipaumbele suala la kulindwa Masjidul Aqswa, wanashabikia na kupanga mikakati ya kuwaua Waislamu wa Iraq, Syria, Afghanistan Pakistan na Lebanon. Amesema, kwa muda wa miaka miwili sasa, makumi ya mamia ya wananchi wa Syria wameuawa kutokana na mashambulio yanayofanywa na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na serikali za Saudi Arabia, Qatar na Uturuki. Amesema kuwa, moja kati ya mikakati ya utawala wa Kizayuni wa Israel ni kuishinikiza Syria iache kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na muqawamah. Sayyid Hassan Nasrullah amelielezea shambulio la hivi karibuni la ndege za Israel dhidi ya Syria kwamba lilikuwa na lengo la kudhoofisha muqawamah, kwa vile Damascus iko mstari wa mbele katika kukabiliana na Wazayuni. Amesisitiza kuwa, kamwe Syria haitaweka chini silaha za muqawamah, bali itaendelea kusimama kidete katika mapambano yake dhidi ya Wazayuni maghasibu.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO