Waasi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wametangaza kusitisha mashambulizi yao dhidi ya askari wa serikali. Habari kutoka Goma, makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini zinasema kuwa, waasi wa Mashariki mwa nchi hiyo, wametangaza hatua hiyo leo baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Jim Yong Kim Mkuu wa Benki ya Dunia, kutembelea eneo la mapigano huko mashariki mwa Kongo DRC.
Msemaji wa kundi la M23 Amani Kabasha, amewaambia waandishi wa habari kuwa, lengo la usitishaji mapigano, ni kuandaa mazingira ya amani mjini Goma kwa ajili ya safari ya Ban Ki-moon.
Tangazo hilo la usitishaji mapigano, linatolewa katika hali ambayo, siku kadhaa zilizopita kumeshuhudiwa mapigano makali karibu na mji wa Goma katika mpaka wa nchi hiyo na Rwanda.
Hapo jana Katibu Mkuu ya Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo mjini Kinshasa. Safari ya Ban nchini Kongo inafanyika katika fremu ya safari yake ya kulitembelea eneo la Maziwa Makuu la Afrika.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO