Viongozi wa nchi mbali mbali duniani wameanza kumpongeza Hassan Rohani kwa ushindi wake mkubwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika Ijumaa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amempongeza Rohani na kusema anatarajia kushirikiana na Iran kuhusu masuala muhimu ya kimataifa. Ban pia ameelezea kufurahishwa kwake na kujitokeza asilimia 72 ya watu wa Iran katika uchaguzi wa rais. Rais Hamid Karzai wa Afghanistan pia amempongeza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na taifa la Iran kufuatia ushindi wa Rohani. Karzai ametaka uhusiano wa Iran na Afghanistan uimarishwe katika serikali mpya. Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Carl Bildt amempongeza Rohani kwa ushindi wkae na kusema nchi yake inataka kuboresha uhusiano na Iran. Kwa upande wake, Catherine Ashton Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya amempongeza Rohani kwa ushindi wake na kusema umoja huo una azma ya kushirikiana na serikali mpya ya Iran katika kutatua kadhia ya nyuklia kwa njia za kidiplomasia. Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Bi. Emma Bonino sambamba na kutoa salamu za pongezi kufuatia ushindi wa Hassan Rohani amesema kushiriki kwa wingi watu wa matabaka mbali mbali ya Iran katika uchaguzi ni jambo linaloashiria uhalali wa juu wa rais mpya. Ufaransa na Ujerumani pia zimetoa taarifa za kumpongeza rais-mteule wa Iran kwa ushindi wake na kutangaza kuwa tayari kushirikiana zaidi na Tehran.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO