Marekani na Umoja wa Ulaya zimeanzisha majadiliano kwa ajili ya eneo huru la bishara wakati wa kuanza kwa mkutano wa mataifa tajiri duniani ya G8 nchini Ireland ya kaskazini. Akizungumza katika mkutano mjini Enniskillen , rais wa Marekani Barack Obama amesema kuwa duru ya kwanza ya mazungumzo hayo itafanyika mjini Washington Julai. Biashara kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya kwa hivi sasa inathamani ya karibu euro bilioni mbili na robo kwa siku, lakini wadadisi wanasema ushirikiano wa kimya kimya wa kibiashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo yanayopakana na bahari ya Atlantic yanaweza kuongeza biashara hiyo kwa kiasi cha euro bilioni 100 kwa mwaka kwa kila upande. Wazo hilo la makubaliano kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya lilianza kufikiriwa miongo kadha iliyopita lakini ilizuiliwa na Ufaransa katika miaka ya 1990. Wazo hilo limepata msukumo mpya sasa wakati pamde hizo mbili zikitafuta ukuaji wa binafsi, pamoja na kujilinda dhidi ya China. Marekani na halmashauri ya umoja wa Ulaya , chombo kitendaji cha umoja wa mataifa 27 ya Ulaya , zinatarajia kukamilisha makubaliano hayo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO