Saturday, June 29, 2013

IRAN KUJENGA KITUO KIPYA CHA NYUKLIA

Dakta Fereydun Abbasi Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina mpango wa kujenga kituo kipya cha nyuklia. Akizungumza na waandishi wa habari wa kigeni katika mji wa Saint Petersburg nchini Russia, Dakta Abbasi ameongeza kuwa, eneo la kujengwa kituo hicho kipya limeshatengwa, na hivi karibuni Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA utajulishwa juu ya mpango huo. Abbasi ambaye anahudhuria maonyesho ya kimataifa ya Atom - Expo 2013 na kikao cha nishati ya umeme wa nyuklia katika karne ya 21 mjini Saint Petersburg ameongeza kuwa, mikakati ya Iran ilikuwa ni kujenga tanuri la nyuklia lenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 1,000 hadi 1,200 huko Bushehr, ambapo moja kati ya miradi hiyo miwili tayari umeshaanza kufanya kazi. Akizungumzia uwezekano wa kubadilishwa siasa za nyuklia za Iran baada ya kuingia madarakani serikali ya Dakta Hassan Ruhani, Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran amesema kuwa, shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa malengo ya amani kwa minajili ya kudhamini nishati ya umeme na kuondoa mahitajio kwa wananchi na kwamba hakuna mabadiliko yoyote ya kimsingi yatakayofanyika.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO