Saturday, June 01, 2013

ISRAEL YAEMEWA JUU YA MAKOMBORA MAPYA YA SYRIA

John Kerry Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani amesema kuwa, hatua ya Russia ya kuipatia Syria mfumo wa kukabiliana na mashambulizi ya makombora aina ya S-300 imewatia kiwewe viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Akizungumza akiwa pamoja na Guido Westerwalle Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Kerry amesisitiza kuwa, kutumwa kwa mitambo hiyo ya kuzuia mashambulizi ya makombora bila shaka kutasababisha usalama wa Israel kuwa hatarini. Naye Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani amesema kuwa, Russia imetenda kosa kubwa kwa kuipatia serikali ya Syria mitambo ya kuzuia mashambulizi ya makombora. Hata hivyo Russia imetangaza kuwa, mkataba wa kuipatia Syria mitambo ya kukabiliana na mashambulizi ya makombora aina ya S–300 ulitiwa saini mwaka 2010, kabla hata  ya kuanza machafuko nchini Syria, kwa minajili hiyo Moscow inapaswa kuheshimu na kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili. Matamshi ya viongozi hao wa Marekani na Ujerumani yanatolewa katika hali ambayo, Umoja wa Ulaya hivi karibuni uliondoa vikwazo vya silaha kwa wapinzani na magaidi wa Syria wanaofanya mauaji ya kiholela dhidi ya wananchi na maafisa wa serikali nchini Syria.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO