Saturday, June 15, 2013

MUGABE ATANGAZA SIKU YA UCHAGUZI

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ametangaza kuwa, uchaguzi wa nchi hiyo utafanyika tarehe 31 Julai mwaka huu. Duru za kuaminika kutoka mjini Harare zimethibitisha habari hiyo, lakini hazikuelezea zaidi kuhusiana na kadhia hiyo. Kutangazwa tarehe hiyo, kunajiri katika hali ambayo, hapo jana Waziri Mkuu wa nchi hiyo Morgan Tsvangirai alikuwa ametangaza kuwa, chama chake cha MDC kitapinga kufanyika uchaguzi huo ikiwa hakutafanyika marekebisho yaliyoainishwa, yanayohusu kufanyika kwa uchaguzi huru na wa demokrasia nchini humo. Uchaguzi huo unatarajiwa kumaliza uongozi wa serikali ya umoja wa kitaifa, iliyoundwa mwaka 2009 kwa mashinikizo ya kimataifa ambayo inavishirikisha vyama vya ZANU-PF kinachoongozwa na Rais Mugabe na kile cha MDC, kinachoongozwa na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai. Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilielezea wasiwasi wake kuhusu hatua ya baadhi ya maafisa wakuu wa usalama nchini Zimbabwe kujiingiza katika masuala ya kisiasa na kuonya kuwa jambo hilo linaweza kutatiza uchaguzi mkuu ujao nchini humo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO