Dakta Hassan Rohani Rais Mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo amekutana na kufanya mazungumzo na Dakta Ali Larijani Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani bunge na wamesisitiza juu ya udharura wa kuimarishwa mashirikiano ya mihimili hiyo miwili ya dola kwa lengo la kutatua matatizo ya wananchi wa Iran. Viongozi hao wawili wameeleza kuwa, hivi sasa kunahitajika mashirikiano na fikra za pamoja za pande mbili katika kutatua matatizo yanayolikabili taifa la Iran. Dakta Rohani amesema kwenye mazungumzo na waandishi wa habari kwamba, furaha iliyoonyeshwa na wananchi wa Iran mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais, ni dalili tosha kuwa wananchi wana matumaini makubwa katika siku za usoni. Taarifa zinasema kuwa, kesho Jumatatu Dakta Hassan Rohani atakuwa na kikao na waandishi wa habari na kutangaza mikakati ya serikali yake ijayo katika masuala ya ndani na kimataifa. Rais Mteule atachukua jukumu rasmi la kuiongoza nchi tarehe 3 Agosti mwaka huu baada ya kutawazwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO