Wednesday, June 05, 2013

UN YATAKA KUSITISHWA KUTUMWA SILAHA SYRIA

Waasi  nchini  Syria  wamekiri jana  kuwa  wameupoteza mji muhimu   wa  Qusayr , baada  ya  jeshi la  nchi  hiyo kudai  linaudhibiti  mji  wote  pamoja  na  maeneo yanayozunguka  mji  huo. Shirika  linaloangalia  haki  za binadamu  nchini  Syria  limesema  wapiganaji  kutoka kundi  la  Hezboullah  nchini  Lebanon , kundi  ambalo limesaidia mashambulizi  ya majeshi  ya serikali, linaudhibiti mji  huo.
Wakati  huo  huo  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa Ufaransa Laurent Fabius  amesema  kuwa  anauhakika silaha  za  kemikali  zimetumika  nchini  Syria. Matamshi hayo  yanakuja  wakati  Umoja  wa  Mataifa  umetoa  ripoti inayoonyesha  hali  kuwa  mbaya   katika  vita  vya wenyewe  kwa  wenyewe  nchini  Syria.  Akizungumza katika televisheni , waziri  Fabius ametupa  lawama za mashambulizi  hayo  kwa   utawala  wa  rais  Bashar al-Assad.
Wakati  huo  huo  Uingereza  nayo  imesema  leo  kuwa utafiti  uliofanywa kuhusu  matumizi  ya  gesi  ya  sarin nchini  Syria  umeonesha  kuwa  gesi  hiyo  imetumika  na taarifa   zinaonesha  kuwa  majeshi  ya  serikali  yanatumia silaha  za  kemikali.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO