Serikali mpya ya Misri imeanza kazi leo ikikabiliwa na changamoto kubwa ikiwa ni pamoja na kurejesha usalama, wakati wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani, Mohamed Mursi, wakiandamana kupinga utawala wa mpito. Zaidi ya waandamanaji 1,000 walikusanyika hatua chache kutoka makao makuu ya baraza la mawaziri, karibu na uwanja wa Tahrir mjini Cairo, wakipiga kelele za kuipinga serikali. Maandamano hayo yamekuja wakati Mkuu wa sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, akianza msururu wa mikutano mjini Cairo na viongozi wapya wa Misri, ikiwa ni pamoja na Rais Adly Mansour na Makamu wa rais, Mohammed El Baradei. Katika mazungumzo hayo, Ashton amesema Umoja wa Ulaya unataka nchi hiyo irudi haraka katika utawala wa kidemokrasia na kuzishirikisha pande zote za kisiasa. Pia alisisitiza kuhusu haja ya kuufufua uchumi haraka iwezekanavyo. Chama cha Mursi cha Udugu wa Kiislamu, na chama cha kihafidhina cha Al-Nur, vimekataa kushiriki katika serikali hiyo mpya.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO