Thursday, July 18, 2013

KERRY AKUTANA NA MAAFISA WA JUMUIYA YA WAARABU

Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani, John Kerry, leo amekutana na maafisa wakuu wa Jumuiya ya Kiarabu na kuwafahamisha kuhusu juhudi zake za kuanzisha upya mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina. Pia amewafahamisha kuhusu maoni ya Marekani kuhusu migogoro inayoendelea nchini Syria na Misri. Ikiwa ni ziara yake ya sita katika eneo hilo katika kipindi cha miezi kadhaa, Kerry amekutana nchini Jordan na wawakilishi wa Jumuiya ya Kiarabu na wanachama wake tisa, ambao wanaunga mkono mpango mpana wa amani kati ya nchi za Kiarabu na Israel uliopendekezwa na Saudi Arabia. Pia amewafahamisha maafisa hao kuhusu uungaji mkono wa Marekani kwa upinzani wa Syria na juhudi za kuandaa kongamano la kimataifa ili kuunda nchini humo serikali ya mpito pamoja na msimamo wa Marekani katika mzozo wa kisiasa wa Misri. Kikao hicho kinakuja siku moja baada ya Kerry kufanya mazungumzo ya chakula cha jioni na Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, ambayo yalidumu kwa saa tano.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO