Thursday, July 18, 2013

SNOWDERN KUONDOKA UWANJA WA NDEGE MOSCOW

Aliyekuwa wakala wa shirika la ujasusi la Marekani, Edward Snowden, huenda hivi karibuni akaondoka katika uwanja wa ndege wa Moscow nchini Urusi, ambako amekuwa akijificha kwa zaidi ya wiki tatu. Wakili wake Mrusi, Anatoly Kucherena, amesema Snowden ataweza kuondoka katika eneo la abiria la uwanja huo wa Sherementyevo katika siku chache zijazo. Mmarekani huyo amekwama katika uwanja huo tangu Juni 23 kwa sababu Marekani imebatilisha paspoti yake. Hapo jana aliwasilisha ombi rasmi la kupewa hifadhi nchini Urusi. Kucherena pia amesema Snowden hajafutilia mbali uwezekano wa kuomba uraia wa Urusi. Wakili huyo amesema Snowden anasema kuondoka uwanjani humo punde Ofisi ya Uhamiaji ya Urusi itakapomkabidhi cheti kinachosema kuwa ombi lake la kupewa hifadhi linatathminiwa. Mapema leo, Rais wa nchi hiyo, Vladmir Putin, amesema Snowden ameonywa kwamba Urusi haitavumilia vitendo vyovyote vitakavyohujumu uhusiano kati ya Urusi na Marekani. Amesema uhusiano wa kimataifa ni muhimu kuliko ugomvi unaoyahusisha mashirika ya kijasusi.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO