Mahmoud Abbas Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amefanya mazungumzo na Rais Michel Suleiman wa Lebanon mjini Beirut na kusisitiza kuwa, suala kurejea wakimbizi wa Kipalestina kwenye ardhi zao za asili, ni jambo linalopewa kipaumbele na Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Rais Mahmoud Abbas ameishukuru serikali na wananchi wa Lebanon kwa ukarimu wao wa kuwapokea zaidi ya wakimbizi laki nne wa Kipalestina ambao walikimbilia nchini humo baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina. Ameongeza kuwa, makazi ya wakimbizi wa Kipalestina nchini Lebanon na katika nchi nyingine duniani ni ya muda, na Mamlaka ya Ndani ya Palestina itaendeleza juhudi zake za kuwarejesha wakimbizi wote wa Kipalestina kwenye ardhi na makazi yao ya asili. Mahmoud Abbas amesisitiza kuwa, ni jukumu la serikali ya Lebanon kutoa maamuzi juu ya silaha zinazomilikiwa na wakimbizi wa Kipalestina kwenye kambi za wakimbizi nchini Lebanon. Imeelezwa kuwa, zaidi ya wakimbizi laki nne wa Kipalestina wanaishi nchini Lebanon ambapo viongozi wa serikali ya Beirut wanaeleza kuwa kuendelea kubaki wakimbizi hao nchini humo kumesababisha matatizo mengi kwa nchi hiyo na hasa katika masuala ya kiusalama. Taarifa zinasema kuwa, moja kati ya matatizo makubwa yanayoikumba nchi hiyo, ni suala la silaha zinazomilikiwa na wakimbizi wa Kipalestina kwenye kambi wanazoishi, kwani kwa upande mmoja suala la kudhaminiwa usalama wa kambi hizo liko mikononi mwa makundi ya Kipalestina na kwa upande wa pili kuwepo lundo la silaha kwenye mikono ya baadhi ya makundi ambayo hayastahili kumiliki silaha hizo kumesababisha ukosefu wa usalama na hata kujitokeza mapigano ndani na nje ya kambi hizo za wakimbizi. Satua na ushawishi wa makundi ya Kiwahabi yenye misimamo mikali yenye kuwakufurisha Waislamu wengine ndani ya kambi hizo, ni moja pia ya matatizo yanayoikumba serikali ya Lebanon. Kwa mujibu wa ripoti za viongozi wa Kipalestina na Umoja wa Mataifa, hivi sasa imepindukia zaidi ya wakimbizi milioni tano wa Kipalestina wanaoishi katika nchi za Lebanon, Jordan, Misri na Syria baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kukataa kurejea wakimbizi hao kwenye ardhi zao za asili. Wimbi la kuwafukuza Wapalestina kwenye ardhi zao za asili lilianza mwaka 1948 baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kutekeleza siasa na sera za kuwashinikiza na kuwafukuza Wapalestina kwenye ardhi zao za asili. Viongozi wa Israel ambao wanapinga vikali kurejeshwa wakimbizi wa Kipalestina kwenye ardhi zao, daima wamekuwa wakitekeleza siasa za mauaji ya kizazi cha Wapalestina, ili wananchi wengine wa Kipalestina waweze kuyakimbia makazi yao ya asili. Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa azimio nambari 194 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la tarehe 11 Disemba 1948, wakimbizi wa Kipalestina wana haki kikamilifu ya kurejea kwenye ardhi zao za asili zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO