Rais Evo Morales wa Bolivia ambaye ndege yake ilinyimwa ruhusa ya kutumia anga ya Ufaransa na Ureno na kuhatarisha usalama wake, amepokelewa leo kishujaa na wananchi wa nchi hiyo. Hapo juzi nchi za Ufaransa, Ureno na Uhispania ziliinyima ruhusa ndege iliyokuwa imembeba Rais Morales, kutumia anga yao wakati rais huyo akirejea nyumbani baada ya kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa nishati huko nchini Russia na kulazimika kutua kwa dharura nchini Austria. Nchi hizo zilidai kuwa, hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na hitilafu za kiufundi huku duru za habari zikianika wazi kuwa hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kushuku kuwa, huenda Rais Morales alikuwa ameandamana na Edward Snowden afisa wa zamani wa CIA ya Marekani anayesakwa kwa udi na uvumba na Washington. Kufuatia hali hiyo, ndege ya rais huyo ilibakia katika uwanja wa ndege wa Austria kwa muda wa masaa 10, hadi baada ya serikali za Ufaransa, Italia, Ureno, na Uhispania kutoa idhini ya kuvuka kwenye anga za nchi hizo, ndipo akafanikiwa kuelekea nchini kwake. Serikali na wananchi wa Bolovia wamelaani vikali hatua hiyo na kuitaja kuwa ilifanyika kwa lengo la kumvunjia heshima na kuhatarisha maisha ya rais huyo. Edward Snowden, jasusi wa zamani wa Marekani anasakwa na nchi yake baada ya kufichua kuwa CIA na mashirika mengine ya kijasusi ya Washington yamekuwa yakifanya ujasusi dhidi ya watu kote duniani wakiwemo wanadiplomasia na viongozi wa Ulaya, kwa kusikiliza kwa siri mazungumzo yao ya simu na kudukua baruapepe zao.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO