Saturday, July 20, 2013

MAREKANI YAISHUTUMU RUSSIA KUTOKANA NA SILAHA ZA KIKEMIKALI

Viongozi wa Russia wamekasirishwa mno na ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani kuhusiana na udhibiti na utokomezaji wa silaha za kemikali. Wizara hiyo imeituhumu Russia kwamba haitekelezi ipasavyo makubaliano ya kuangamiza silaha hizo. Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Russia imetoa radiamali kali na kuikosoa Marekani kwamba imetoa taarifa hiyo bila kuzingatia sababu za kimsingi na kwenda kinyume na makubaliano ya kuzuia utumiaji wa silaha za kemikali. Makubaliano ya kuzuia kuzalisha, kutumia na kulimbikiza silaha za kemikali yalifikiwa kutokana na juhudi za miaka kadhaa za jamii ya kimataifa za kuzuia uzalishaji na utumiaji wa silaha hizo  za maangamizi. Taasisi ya Kuzuia Silaha za Kemikali, yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, ina jukumu la kisheria la kutekeleza makubaliano hayo ya kimataifa. Russia na Marekani ni miongoni mwa nchi wanachama 188 wa taasisi hiyo. Nchi hizo mbili kama ilivyo kwa wanachama wengine, zinapaswa kuangamiza viwanda vyao vya kemikali hatua kwa hatua. Washington na Moscow zinahesabiwa kuwa wamiliki wakubwa wa viwanda vya kemikali duniani na kiwango cha silaha zao za kemikali kinatishia amani ya mabara yote ulimwenguni.  Hadi kufikia mwaka 2010, Marekani ilikuwa imeshatokomeza karibu asilimia 75 ya silaha zake za kemikali. Russia nayo hadi kufikia mwezi Aprili 2012, ilikuwa imeshaharibu asilimia 62 ya silaha hizo. Hata hivyo, Moscow inadai kuwa, hadi kufikia sasa tayari imeshatokomeza asilimia 74 ya silaha zake za kemikali. Kabla ya hapo, Russia iliiomba Taasisi ya Kuzuia Silaha za Kemikali kuiongezea muda wa kutokomeza silaha hizo hadi kufikia mwaka 2015, badala ya muda ulioainishwa awali na taasisi hiyo ya kimataifa wa kuzitaka nchi zote wanachama  kutokomeza silaha zao kufikia mwishoni mwa  mwaka 2012. Aidha Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Russia imeeleza kwenye ripoti yake kwamba, tuhuma kama hizo za Washington zinapoteza hali ya kuaminiana kati ya nchi hizo mbili. Ripoti ya Russia pia imeelezea wasiwasi wake kuhusiana na shughuli za bioteknolojia zinazofanywa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani karibu na mipaka ya Russia. Vyombo vya kidiplomasia vya Russia pia vinaikosoa Marekani kwamba, haitoi fursa kwa Taasisi ya Kuzuia Silaha za Kemikali kufanyika utaratibu wa kusimamia na kupata ripoti za uhakika kutoka kwa nchi wanachama wa taasisi hiyo. Kwa utaratibu huo inaonekana kuwa nchi mbili hizo bado zinaathiriwa na mazingira ya kipindi cha Vita Baridi kwani bado zinahisi hatari kutoka upande wa pili, jambo ambalo linaendelea kuathiri uhusiano wao.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO