Serikali ya Marekani imetangaza kwamba, iwapo Russia itamkabidhi Edward Snowden kwa serikali ya Washington, haitamuhukumu adhabu ya kifo, kwa tuhuma za kufichua siri na nyaraka za Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani NSA. Eric Holder Mwanasheria Mkuu wa Marekani amemuandikia barua Alexander Vladimirovich Konovalov Waziri wa Sheria wa Russia na kumuhakikisha kwamba, Snowden hatateswa wala hatakabiliwa na adhabu ya kifo. Kwa muda wa wiki kadhaa sasa Snowden yuko kiwanja cha ndege cha Moscow, lakini wiki iliyopita aliomba hifadhi ya muda ya ukimbizi nchini Russia.
Edward Snowden afisa wa zamani wa shirika la usalama wa taifa la Marekani NSA alifichua kwamba Washington imekuwa ikifanya ujasusi wa kimataifa kwa kudukua baruapepe za wote duniani pamoja na kusikiliza mazungumzo ya simu kwa siri, jambo lililaaniwa na nchi mbalimbali duniani. Wakati huohuo, Baraza la Seneti la Marekani limetangaza kuwa, iwapo serikali ya Russia itampatia hifadhi ya ukimbizi Edward Snowden, kuna uwezekano kwa nchi hiyo kukabiliwa na vikwazo vya kibiashara kutoka Washington.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO