Sunday, July 28, 2013

WAPINZANI SYRIA WATAKA ASSAD KUSHINIKIZWA MABADILIKO

Muungano Mkuu wa wapinzani nchini Syria umeliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC kumshinikiza Rais Bashar al-Assad kukubali kuingia katika makubaliano ya kumaliza machafuko ya kisiasa yaliyodumu kwa zaidi ya miaka miwili wakati wa utawala wake. Mkuu mpya wa Muungano huo Ahmad Jarba ameliambia baraza la usalama kuwa shinikizo zaidi toka jumuiya ya kimataifa linahitajika ili serikali ya Assad ikubali kwenda sambamba na mabadiliko ya kisiasa. Aidha wapinzani hao wametaka jumuiya ya kimataifa kuishinikiza Urusi kusitisha msaada wa silaha kwa serikali ya Assad.
Wapinzani wa Rais Assad wapo katika ziara ya kuweka bayana malengo yao juu ya mgogoro wa Syria sambamba na kuomba msaada wa silaha kwa mataifa ya Magharibi. Hata hivyo mkutano wa kwanza kati ya Muungano wa wapinzani wa Syria na wanachama 15 wa baraza la usalama la umoja wa mataifa haujaonyesha dalili za mafanikio ya kusaka suluhu ya mgogoro huo ambao kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa UN umesababisha mauaji ya watu zaidi ya laki moja toka yalipoanza mwanzoni mwa mwaka 2011.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO