Friday, July 12, 2013

MSAFARA WA AMISON WASHAMBULIWA MOGADISHU

Kwa akali watu watatu wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, baada ya bomu la kutegwa garini lililoulenga msafara wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM kulipuka mjini Mogadishu.
Hili linahesabiwa kuwa shambulio jipya dhidi ya vikosi vya AMISOM katika barabara yenye msongamano mkubwa wa watu pambizoni kidogo mwa mji wa Mogadishu. Duru za habari zinasema kuwa, baada ya kutokea mlipuko huo, zilisikika sauti za silaha nzito katika eneo hilo. Naibu Meya wa Mogadishu ameviambia vyombo vya habari kwamba watu watatu akiwemo mtegaji wa shambulio hilo, wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa. Naibu Meya wa Mogadishu ameongeza kuwa, hakuna hata askari mmoja wa AMISOM aliyeuawa au kujeruhiwa kwenye shambulio hilo.
Hadi sasa hakuna kundi lolote lililojitangaza kuhusika na shambulio hilo lililofanyika leo, lakini kundi la al Shabab limekuwa likijitangaza kuhusika na mashambulio kama hayo dhidi ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika nchini Somalia.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO