Rais François Hollande wa Ufaransa ameutaka Umoja wa Ulaya kuchukua hatua kali na za pamoja dhidi ya Marekani kutokana na vitendo vyake vya ujasusi. Hollande ameyasema hayo wakati alipokutana na rais mwenza wa Lithuania, Bi Dalia Grybauskaitė ambaye nchi yake ndiye mwenyekiti wa umoja huo na kutaka kuchukuliwa hatua kali za pamoja kuhusiana na vitendo vya ujasusi vya Washington dhidi ya viongozi wa Ulaya. Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa ameitaka EU kuihoji serikali ya Washington kuhusiana na vitendo vyake hivyo. Manuel Valls amesema, Paris inasubiri majibu yaliyo wazi kutoka kwa Marekani kuhusiana na matamshi ya EdwardJoseph Snowden na vitendo vya kijasusi wa Washington dhidi ya nchi za Ulaya. EdwardSnowden ni mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA aliyefichua siri ya ujasusi huo. Hivi karibuni afisa huyo wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA, Edward Snowden, aliliambia jarida la kila wiki la Der Spiegel la nchini Ujerumani kwamba, mwaka uliopita wa 2012, Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA) liliwafanyia ujasusi baadhi ya wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya (EU) kwenye ofisi za umoja huo katika miji ya Washington, New York na Brussels. Snowden alisema kuwa, katika ujasusi huo maafisa wa ujasusi wa Marekani waliweka vinasa sauti pamoja na kamera za siri sambamba na kudukua barua-pepe za wanadiplomasia hao.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO