Wizara ya Ulinzi ya Russia imeanza manuva makubwa ya vikosi vyake ya kijeshi huko mashariki mwa nchi hiyo. Manuva hayo yatakayoendelea hadi tarehe 20 Julai, yanawashirikisha askari elfu 80, magari ya deraya elfu moja, ndege 130 na meli 70 za kivita. Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kuwa, lengo la luteka hiyo, ni kufanyia majaribio kiwango cha maandalizi ya vikosi vya kijeshi katika kutekeleza majukumu yake na kupima hali ya mafunzo na utayari wa kiufundi wa jeshi la nchi hiyo. Hii ni luteka kubwa kuwahi kufanywa na jeshi la Russia kwa shabaha ya kupima uwezo wa utayari wa vikosi vya jeshi lake tangu kusambaratika Umoja wa Kisovieti. Kwa upande mwingine na kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO, ni kwamba NATO itafanya manuva makubwa ya kijeshi katika majira ya kipupwe mwakani ambayo yatahesabiwa kuwa manufa makubwa zaidi kuwahi kufanywa na NATO katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Katika manuva hayo, NATO inaazimia kuzishirikisha nchi za Lithuania, Latvia, Estonia na Poland katika manuva hayo. Katika upande wa pili, Russia na Belarus nazo zitafanya manuva mingine ya kijeshi iliyopewa jina la ‘Magharibi-2013’ sambamba na manuva hayo ya NATO. Hii ni kusema kwamba, baada ya Rais Vladimir Putin wa Russia kurejea madarakani mwaka 2012, kulianza vita baridi ambavyo vinaweza kutajwa kuwa ni sehemu ya mgogoro uliojitokeza katika uhusiano baina ya Moscow na Washington. Ikumbukwe kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zilizopo hivi sasa ni hatua ya NATO ya kupanua ushawishi wake wa kijeshi kwenye maeneo ya mpakani na Russia na kuwekwa ngao ya makombora huko mashariki mwa Ulaya. Kwa mtazamo wa serikali ya Moscow, Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO ni muungano wa kijeshi ulioundwa kupambana na Umoja wa Kisovieti na kwamba shirika hilo bado ni adui mkubwa wa Russia. Aidha kwa mujibu wa Russia, licha ya mabadiliko yaliyojiri huko Ulaya na ulimwenguni kwa ujumla, bado NATO imebakia kuwa tishio kubwa kwa usalama wa nchi hiyo. Kadhalika Russia inalihesabu sisitizo la Marekani la kuweka mfumo wa kujilinda na makombora katika nchi za Ulaya, kuwa ina lengo la kudhoofisha mfumo wa kujilinda duniani suala ambalo linapingwa vikali na Moscow. Mbali na hayo, Russia inaamini kuwa hatua ya Marekani ya kujiimarisha kwa silaha za kisasa za mauaji ya umati yakiwemo mabomu ya mauaji ya umati ya nyuklia ni hatati kwa usalama wake. Inaonekana ni kutokana na siasa hizo za kupenda kujitanua za Marekani, ndio maana Russia ikaazimia kufanya manuva matatu makubwa ya kijeshi mwaka huu ambayo inayataja kuwa makubwa zaidi kuwahi kufanywa katika historia ya nchi hiyo. Aidha katika luteka hizo Russia inakusudia kuonyesha uwezo wake mkubwa kimataifa.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO