Thursday, July 18, 2013

SHEHENA YA SILAHA TOKA CUBE KWENDA KOREA KASKAZINI YAKAMATWA

Serikali ya Cuba imekiri kuwa meli ya Korea Kaskazini iliyokamatwa nchini Panama ilikuwa na silaha za kujihami zilizokuwa zinapelekwa nchini humo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Cuba, imekiri meli hiyo kuwa na shehena ya sukari ya zaidi ya tani elfu moja pamoja na silaha za kujihami 240 ambazo korea kaskazini iliziomba. Miongoni mwa silaha ambazo zimekamatwa ni pamoja na mitambo ya kudungulia ndege, maroketi na ndege moja ya kivita aina ya G21 ambazo kwa sehemu zilikuwa ni vifaa vya kukarabati silaha za ulinzi za Korea Kaskazini. Rais wa Panama, Ricardo Martinelli amesema maofisa usalama wa nchi hiyo waliikamata meli hiyo baada ya kuhisi kuwa ilikuwa imesheheni silaha za hatari ambazo zimepigwa marufuku kuingia nchini Korea Kaskazini.
Serikali ya Cuba imeendelea kusisitiza kuwa shehena hiyo ya silaha ni sehemu ya makubaliano kati yake na Korea Kaskazini katika ushirikiano wa kiusalama hasa kwenye mataifa yao na kutaka suala hilo lisichukuliwe kisiasa. Rais wa Panama ameongeza kuwa ni lazima dunia kwa sasa isiruhusu usafirishwaji wa silaha kama hizi kwa siri na hasa kupitia ukingo wake wa bahari yake ya Atlantica. Msemaji wa kitengo cha polisi wa kupambana na dawa za kulevya nchini humo ambaye alishiriki kwenye operesheni hiyo, amesema kuwa wafanyakazi wa meli hiyo walijaribu kukabiliana na askari wake kabla ya kuruhusu meli yao kukaguliwa. Serikali ya Marekani kupitia msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Patrick Ventrell imepongeza uamuzi wa Panama kuisimamisha meli hiyo na kuikagua na kwamba taifa hilo liko tayari kutoa msaada iwapo utahitajika.
Nchi ya Marekani imekuwa kinara wa kupinga Korea Kaskazini kupatiwa silaha za kijeshi huku ikiwa inakabiliwa na vikwazo ambavyo vimewekwa na Umoja wa Mataifa kutokana na mpango wake wa kurutubisha Nyuklia.Mamlaka nchini Panama zimesema zinaendelea kuwahoji wafanyakazi wa meli hiyo akiwemo nahodha wake ambaye awali alipata mshtuko wa moyo na kisha kutaka kujiua kabla ya kukamatwa na askari. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema hatua hiyo imekiuka maazimio ya baraza la Usalama ya kuiwekea vikwazo vya silaha nchi ya Korea Kaskazini na kwamba hatua hii pia itaharibu uhusiano kati ya Serikali ya Havana na Washington.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO