Viongozi wa Amerika ya Kusini wameitaka Marekani iache mpango wake wa udukuzi wa njia za mawasiliano katika kanda yao.Rais wa Argentina Cristina Fernandez ameulezea mpango huo unaodaiwa kufanywa na Marekani wa kufuatilia mawasilano ya mitandaoni kama ukoloni mambo leo. Viongozi hao pia wamesisitiza haki yao ya kuridhia kumpa hifadhi mfichua siri za Marekani Edward Snowden.
Snowden aliwaambia wanaharakati katika uwanja wa ndege wa Moscow kuwa anatumai kukaa Urusi hadi pale atakapopata njia salama ya kuelekea Amerika ya kusini.
Utawala wa Marekani umesema umetamaushwa na kuwepo kwa mkutano huo. Msemaji wa Ikulu ya Rais Jay Carney amesema kumpa Snowden jukwaa la kueneza propaganda kunakinzana na msimamo wa awali wa Urusi kuwa haitaegemea upande wowote katika suala hilo na kuwa hawana ushawishi wa kuwepo kwake katika uwanja huo wa ndege na pia ni kinyume na hakikisho la Urusi kuwa hawatamtaka Snowden kuendelea kuharibu maslahi ya Marekani . Wakati huo huo Rais Barrack Obama amezungumza na Rais wa Urusi Vladimiri Putin kwa njia ya simu muda mfupi baada ya ikulu ya Marekani kuionya Urusi kutompa Snowden jukwaa la kueneza propaganda kwa kumpa hifadhi.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO