Makundi ya kutetea haki za kibinadam yameishutumu serikali ya Nigeria, kwa kumualika rais wa Sudan, Omal al-Bashir, nchini Nigeria na wameitaka jeshi la nchi hiyo kumkamata rais huyo wa Sudan. Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, imetoa kibali cha kukamatwa kwa rais huyo kwa Sudan kwa tuhumu za kuhusika na mauaji ya halaiki. Rais Bashir anahudhuria mkutano wa viongozi wa serikali za nchi za Muungano wa Afrika AU, kuhusu afya mjini Abuja. Makundi hayo ya kutetea haki za kibinadam yamesema kuwa, ziara hiyo ni dharua kwa wahanga wa mzozo huo unaoendelea katika eneo la Darfur.
Rais Bashir amekanusha mashtaka hayo yanayomkabili mbele ya mahakama ya ICC. Mwaka wa 2009, baada ya ICC kutoka kibali cha kukamatwa kwa Bwana Al Bashir, viongozi wa serikali wa Muungano wa Afrika kwa kauli moja waliafikiana kuwa hawatatekeleza agizo hilo la kumkamata Bwana Bashir. Muungano wa Afrika umeishutumu ICC kwa kuhujumu juhudi za kuleta amani katika mataifa kadhaa barani Afrika na kuwa mahakama hiyo ilikuwa inawalenga viongozi wa nchi za Kiafrika pekee. Alipowasili mjini Abuja siku ya Jumapili, kuhudhuria mkutano huo utakaojadilia masuala ya kudhibiti magonjwa ya Malaria, Ukimwi na Kifua kikuu barani Afrika, rais Bashir, alilakiwa kwa tahadhimu kuu ambapo alikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na jeshi la nchi hiyo.
Shirika la Human Rights Watch lililo na makao yake mjini New York, limesema kuwa Nigeria, imeharibu sifa yake kwa kuwa taifa la kwanza Magharibi mwa Afrika kumkaribisha rais huyo anayesakwa na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC. Mwenyekiti wa shirika la Muungano unaoshinikiza Nigeria kujiunga na Mahakama ya ICC, Nigerian Coalition for the International Criminal Court (NCICC) Chino Obiagwu, amesema serikali ya nchi hiyo imekiuka majukumu yake kuambatana na sheria za kimataifa.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO