Monday, April 22, 2013

185 WAUAWA KATIKA MAPIGANO NIGERIA

Watu wasiopungua 185 wameuliwa kaskazini mashariki mwa Nigeria katika mapigano kati ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo na wapiganaji wa Boko Haram. Lewa Kole afisa wa serikali za mitaa amemueleza gavana wa jimbo la Borno Kashin Shettima kuwa mapigano yalianza Ijumaa iliyopita huko Baga katika jimbo la Borno na kudumu kwa masaa kadhaa.
Hata hivyo bado haijafahamika ni askari, raia au wanamgambo wangapi wa Boko Haram waliouliwa katika mapigano hayo kwa kuzingatia kuchomwa moto viwiliwili vingi ambavyo havijaweza kutambuliwa, kufuatia moto ulioteketeza karibu mji huo wote. Brigedia Jenerali Austin Edokpaye amesema kuwa raia wengi walitumiwa na wapiganaji wa Boko Haram kama ngao ya binadamu katika mapigano hayo.

MISRI KUMHUKUMU NDUGU WA GHADAFI

Mwendesha mashtaka Mkuu nchini Misri, anakusudia kumpandisha kizimbani mtoto wa ndugu wa dikteta aliyeuawa nchini Libya Kanali Muammar Gaddafi. Ahmed GaddafAl-Dam atapandishwa katika mahakama kuu nchini Misri, kwa tuhuma za kuanzisha mauaji, kupambana na askari wa usalama na kumiliki silaha kinyume cha sheria. Itakumbuwa kuwa, tarehe 19 mwezi Machi mwaka huu, Ahmed GaddafAl-Dam aliwafyatulia risasi Polisi wa Kimataifa Interpol na wa Misri na kumjeruhi mmoja wao, katika oparesheni ya kumtia mbaroni mwana huyo wa ndugu wa Kanali Muammar Gaddafi. Mbali na idara ya mahakama nchini Misri kupinga kumkabidhi Ahmed GaddafAl-Dam kwa serikali ya Libya, imetangaza kumshitaki katika mahakama zake huku ikiwa tayari imekwishatekeleza usaili dhidi yake

POLISI 23 BRAZIL WAFUNGWA KIFUNGO CHA MAISHA

Duru za habari nchini Brazil zinaarifu kuwa, polisi 23 wa nchi hiyo wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha, kwa kosa la kuwaua wafungwa nchini humo. Kwa mujibu wa habari hiyo polisi hao waliohukumiwa kila mmoja kifungo cha miaka 156, walihusika katika mauaji makubwa zaidi dhidi ya wafungwa 111 katika jela moja ya nchi hiyo mnamo mwaka 1992. Aidha polisi hao 23 ni miongoni mwa polisi 26 ambao walihukumiwa hapo jana na kuachiliwa huru watatu kati yao. Maafisa hao wa polisi ambao wengi wao tayari walikuwa wamestaafu, walihusika katika mauaji ya wafungwa katika jela ya Carandiru iliyopo katika mji wa Sao Paulo mwaka huo uliotajwa. Hata hivyo mawakili wa polisi hao walioitaka mahakama ya Sao Paulo kuwapunguzia adhabu wateja wao, walidai mahakamani kuwa, polisi hao waliwafyatulia risasi wafungwa hao baada ya maisha yao kuwa hatarini.

Sunday, April 21, 2013

LUFTHANSA KUFUTA SAARI ZAKE BAADA YA MGOMO WA WAFANYAZI


Shirikal la ndege la Lufthansa la nchini Ujerumani limesema limefuta nyingi ya safari zake za Ulaya, safari za masafa marefu na hata zile za ndani ya nchi hapo kesho kutokana na mgomo wa wafanyakazi wake wa uwanjani pamoja na wale wa ndani ya ndege.  
Taarifa kutoka kwa shirika hilo imesema imewaweka wafanyakazi 20 kati ya 1,650 kuziba pengo la wafanyakazi waliogoma kushughulikia safari za masafa mafupi hapo kesho Jumatatu na kuonya kuwepo kwa athari kubwa kwa safari za masafa marefu. 
Chama cha wafanyakazi kiliitisha mgomo huo wa kutaka asilimia 5.2 ya nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi wa uwanjani 33, 000 wa shirika hilo la Lufthansa baada ya kushindwa kwa duru tatu za mazungumzo ya malipo ya mshahara na viongozi wa shirika hilo.

CHUCK HAGEL ZIARANI ISRAEL


Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amewasili nchini Israel hii leo katika ziara yake ya wiki nzima Mashariki ya kati. Katika ziara hiyo Hagel atajadili wasiwasi wa mpango wa nyuklia wa Iran na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.
Katika ziara yake ya kwanza tangu aliposhika wadhifa huo miezi miwili iliopita waziri huyo pia amepanga kuzungumza na mawaziri wenzake wa eneo hilo juu ya mkataba wa silaha wa euro bilioni 10 utakaozipatia ndege za kijeshi za Marekani pamoja na makombora Israel, Saudi Arabia, na nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu.
Amesema mpango huo wa euro bilioni 10 ni ishara tosha kwa Iran kwamba hatua za kijeshi huenda zikachukuliwa kufuatia mpango wake wa nyuklia. 

MAREKANI KUONGEZA MISAA KWA WAASI WA SYRIA


Marekani imesema kuwa itaongeza mara mbili misaada yake kwa upinzani nchini Syria, ikiwa ni pamoja na vifaa vipya vipya vya kijeshi visivyo vya maangamizi, bila kujali wito wa kuuza silaha au kuingilia moja kwa moja. Katika taarifa yake baada ya mazungumzo kati ya marafiki wa Syria wanaounga mkono upinzani wanaokutana huko Istanbul, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry alisema msaada wa Marekani kwa upinzani itakuwa ni dola milioni 250 
Hapo jana Muungano wa upinzani nchini Syria uliikosoa urusi na kusema kuwa imeachwa kando na historia kwa kuunga mkono serikali ya rais Bashar al Assad na kwamba inajitenga yenyewe katika uwanda wa kimataifa.

SHUGHUI ZA UOKOAJI CHINA ZAKUMBWA NA CHANGAMOTO


Waokozi bado wanajaribu kuendelea na shughuli ya kutafuta manusura na miili zaidi katika eneo la milimani la Lushan Kusini Magharibi mwa China, baada ya tetemeko kubwa la ardhi lenye kipimo cha ritcher 6.6 kukumba eneo hilo hapo jana.
Huku hayo yakiarifiwa idadi ya waliofariki kutokana na tetemeko hilo lililosababisha maporomoko ya udongo imepanda na kufikia 203 huku watu wengine 11,800 wakiwa wamejeruhiwa vibaya. Tetemeko hilo liliharibu barabara na kukata mawasilianio ya simu na umeme katika eneo hilo.
Kwa sasa maelfu ya watu wanaendelea kukaa katika mahema wakiwa na hofu kubwa ya kurudi katika eneo hilo.Tetemeko kama hili lilitokea mwaka wa 2008 katika eneo hilo na kusababisha vifo vya takriban watu 70,000.

WAISLAM WAZUIWA KUJENGA MSIKITI UFARANSA

Waislamu wa mji wa Montrouge nchini Ufaransa wamepanga kufanya maandamano makubwa ya kulalamikia hatua ya manispaa ya mji huo ya kupinga kujengwa msikiti mjini humo. Kituo cha habari ya Echo-Montrouge kimewataka Waislamu wa mji wa Montrouge wa kusini mwa mji mkuu wa Ufaransa, Paris, kujitokeza kwa wingi kwenye maandamano hayo ili kulalamikia hatua ya manispaa ya mji huo ya kuzuia kujengwa kituo pekee cha ibada kwa Waislamu mjini humo. Maandamano hayo yamepangwa kufanyika wiki ijayo yaani Aprili 27, na mkuu wa Jamii ya Waislamu wa Ufaransa, Nabil an Nasri, na mkuu wa jamii ya kupambana na chuki dhidi ya Uislamu, Sami Dabbah, watahutubia waandamanaji na kusisitiza juu ya haki ya Waislamu wa mji huo ya kuwa na msikiti. Jumuiya ya Kudumisha Udugu ya mji wa Montrouge ndiyo iliyoitisha maandamano hayo na imewataka wananchi wote wa Ufaransa kushiriki kwenye maandamano hayo. Ujenzi wa msikiti katika mji wa Montrouge huko Ufaransa ulianza miaka minne iliyopita lakini miezi miwili tu tangu kuanza ujenzi huo, manispaa ya mji huo iliingilia kati na kuzuia kuendelea kujengwa sehemu hiyo ya ibada kwa Waislamu. Waislamu wa Ufaransa walipigania sana haki yao hiyo na mwaka huu wa 2013 wamepewa tena kibali ya kuendelea kujenga msikiti huo lakini hivi sasa pia manispaa ya mji wa Montrouge imeingilia tena kati na kuzuia ujenzi huo kwa madai kuwa Waislamu mjini humo ni wachache hivyo hawana haki ya kuwa na msikiti.

CHINA YAILAUMU MAREKANI KUHUSU HAKI ZA BINADAMU

Serikali ya China imeilaumu vikali Marekani kwa kufumbia macho uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na nchi hiyo katika kila kona ya dunia na badala yake Washington inazituhumu nchi nyingine kukanyaga haki hizo. Taarifa ya Baraza la Mawaziri la China iliyotolewa leo imeongeza kuwa, Marekani imekuwa ikivunja wazi wazi haki za binaadamu kwenye operesheni zake za kijeshi katika kona mbalimbali za dunia na kwa hatua yake ya kuyasaidia kifedha makundi ya waasi ambayo yanavuruga misingi ya kidemokrasia katika nchi mbalimbali duniani. Katika ripoti yake iliyoipa jina "Rekodi ya Haki za Binaadamu Nchini Marekani Mwaka 2012," China imesema pia kuwa, machafuko ya kutumia silaha moto nchini Marekani ni mfano mwingine wa uvunjwaji wa haki za binadamu nchini humo. Imesema, mashambulizi ya kiholela ya kutumia silaha moto yameendelea kuwa tishio kubwa kwa usalama na maisha ya wananchi wa kawaida nchini Marekani. Lawama hizo dhidi ya Marekani zimekuja katika hali ambayo Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa nalo limeilaumu nchi hiyo kutokana na mashambulizi ya ndege zake za kigaidi zisizo na rubani zinazoua watu wa kawaida katika nchi mbali ulimwenguni.

MURSI: USHIRIKIANO NA IRAN SI DHIDI YA NCHI NYINGINE

Rais Muhammad Mursi wa Misri amesema kuwa, siasa za nje za Cairo zinalindwa na maslahi yake ya taifa na kuongeza kuwa uhusiano wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si kwa madhara ya nchi nyingine yoyote ile. Akizungumza na kanali ya televisheni ya al Jazeera hapo jana, Rais Muhammad Mursi wa Misri amebainisha kuwa Iran ni moja ya nchi za Kiislamu duniani na kwamba wakati Misri inapokuwa na uhusiano na Iran, uhusiano huo hauwi dhidi ya nchi yoyote ile. Tehran ilikata uhusiano wake wa kidiplomasia na Misri baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 nchini Iran kufuatia hatua ya Cairo ya kusaini mkataba wa Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel na kumpa hifadhi Mohammad Reza Pahlavi mfalme aliyepinduliwa na wananchi hapa Iran. Hata hivyo uhusiano kati ya Tehran na Cairo umekuwa ukiboreka kufuatia mapinduzi ya wananchi wa Misri ya mwaka juzi yaliyomng'oa madarakani dikteta wa nchi hiyo Husni Mubarak.

BOKO HARAM YATAKA KUFANYA MAZUNGUMZO NA SERIKALI

Kundi la Boko Haram ambalo lilihusika na kuwateka nyara raia saba wa Ufaransa limesema kuwa, kuachiwa huru raia hao ni ishara ya juhudi za kundi hilo za kutaka kufanya mazungumzo na serikali ya Nigeria. Muhammad Marwan mwanachama wa kundi la uasi la Boko Haram la nchini Nigeria ametangaza kuwa kitendo cha kuwaachia huru raia saba wa Ufaransa ambao walitekwa nyara tangu miezi iliyopita huko kaskazini mwa Cameroon karibu na mpaka na Nigeria, kunaonyesha kuwa kundi hilo lina nia ya kufanya mazungumzo na serikali. Marwan amesisitiza pia kwamba, kuachiwa huru raia hao wa Ufaransa kumekuja baada ya mashauriano kati ya wakuu wa Boko Haram kama juhudi za kuanzisha mazungumzo na kurejesha utulivu huko Nigeria. Siku kadhaa zilizopita Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria alisema kuwa kumeundwa kamati ya watu 26 waliopewa jukumu la kuchunguza uwezekano wa kuwasamehe wanachama wa kundi la Boko Haram kwa shabaha ya kurejesha amani nchini humo.

TETESI KUHUSU UCHAGUZI WA RAIS IRAN

WAGOMBEA KITI CHA URAIS IRAN

Huku uchaguzi wa rais ukikaribia nchini Iran, joto la kisiasa linaendelea kupanda baada ya kuwepo tetesi kuhusu uwezekano wa kugombea tena marais wa zamani Akbar Hashemi Rafsanjani na Seyyed Mohammad Khatami.
Kwa mujibu wa Press TV, Mohammad Reza Aref ambaye alikuwa makamu wa kwanza wa rais Khatami amesema atajiondoa iwapo rais huyo wa zamani atagombea urais katika uchaguzi wa mwezi Juni. Hata hivyo mgombea Mohsen Rezaei amesema hatajiondoa hata kama marais wa zamani Rafsanjani na Khatami watagombea. Kwa mujibu wa sheria ya Iran, rais wa zamani anaweza kugombea urais baada ya kupita miaka mitano ya kumalizika muhula wake. Wakati huo huo mbunge mwandamizi Alireza Zakani naye amejitosa katika kinyang'anyiro cha urais nchini. Zakani ambaye ni katibu mkuu wa Jumuiya ya Wafuasi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitangaza uamuzi wake Jumamosi usiku. Aidha waziri wa zamani wa afya Kamran Bagheri Lankarani ametangaza kugombea urais kwa tikiti ya Mrengo wa Waibua Hamasa ya Mapinduzi ya Kiislamu. Wengine waliotangaza nia ya kuwania urais wa Iran ni pamoja na waziri wa zamani wa mambo ya ndani Mostafa Pour-Mohammadi, mwanachama mwandamizi wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo, Hassan Rohani na waziri wa zamani wa mambo ya nje Manoucher Mottaki. Rais Mahmoud Ahmadinejad anamaliza muhula wake wa pili na hivyo kikatiba hawezi kugombea. Uchaguzi wa rais Iran utafanyika Juni 14 na wagombea watajiandikisha kati ya Mei 7 na 11.

NAIBU MKUU WA HIZBULLAH ASEMA WAKO TAYARI KWA NJAMA ZOZOTE ZA ISRAEL NA MAREKANI


Naibu Mkuu wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kwamba, harakati hiyo imejiandaa kikamilifu kwa ajili ya kukabiliana na njama za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Mashariki ya Kati. Sheikh Nabil Qaouq amesema kuwa, kuna haja ya kuendelezwa muqawama dhidi ya maadui na kwamba, muqawama ni dharura ya kitaifa na stratejia kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vya utawala haramu wa Israel ambao unataka kuutumia vibaya mgogoro wa sasa wa Syria.
Sheikh Nabil Qaouq amesisitiza kwamba, katika hali ya hivi sasa Hizbullah iko katika hali nzuri kabisa ya maandalizi, jambo ambalo hata Ehud Barak, waziri wa zamani wa vita wa Israel amelikiri bayana. Naibu Mkuu wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, kama ambavyo muqawama ulipata ushindi mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel utazishinda pia njama za Marekani kwa kuitisha uchaguzi na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini Lebanon.

Saturday, April 20, 2013

MALI KUFANYA UCHAGUZI JULAI

Rais wa mpito wa Mali, Dioncounda Traore amewahakikishia washirika wa kimataifa kwamba nchi yake iko tayari kufanya uchaguzi wa kidemokrasia ifikapo mwezi Julai mwaka huu, kama alivyoahidi. Matamshi hayo ameyatoa kwenye mji mkuu wa Bamako, mwanzoni mwa mkutano wa wajumbe wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi-ECOWAS. Rais Traore amesema kutokana na msaada wa marafiki wa Mali, uchaguzi wa nchi hiyo utafanyika kwa muda uliopangwa. Amesema nchi hiyo inayopambana na waasi wenye itikadi kali za Kiislamu iko salama, ingawa bado juhudi zaidi zinahitajika kuimarisha usalama. Katika tamko lililotolewa mwishoni mwa mkutano huo, wajumbe wamefurahishwa na hatua ya kufanyika kwa uchaguzi wa urais mnamo Julai 7 na wa wabunge utakaofanyika Julai 21.

MSHUKIWA NAMBA 2 WA BOSTON ATIWA NGUVUNI

Polisi nchini Marekani inamshikilia kijana mmoja anayedhaniwa kuhusika na mashambulizi yaliyojitokeza katika mbio za marathon za mjini Boston mapema juma hili. Kijana huyo Dzhokhar Tsarnaev mwenye umri wa miaka 19 alikutwa mafichoni alipokuwa amejihifadhi baada ya mshukiwa mwenzie kuuawa katika majibizano makali ya risasi na polisi umbali wa kilomita kumi kutoka Boston.

Ripoti mbalimbali za vyombo vya habari toka nchini humo zinasema mshukiwa huyo alikutwa amejificha kwenye akiwa na majeraha aliyoyapata katika makabiliano baina yao na polisi ambayo yalipelekea kifo cha kaka yake Tamerlan ambaye ni mshukiwa wa pili katika tukio hilo.

Ndugu hao wawili wanadhaniwa ndio waliotega mabomu mawili karibu na mstari wa mwisho wa mbio za marathon za Boston siku ya jumatatu, tukio ambalo lilisababisha vifo vya watu watatu na wengine zaidi ya 170 kujeruhiwa.

Kamishna wa polisi wa Boston Ed Davis amewaambia waandishi wa habari hali ya mshukiwa huyo ni mbaya sana kutokana na majeraha aliyonayo na anapatiwa matibabu katika hospitali moja mjini humo.

Akizungumza baada ya kukamatwa kwa mshukiwa wa pili, Rais wa Marekani Barack Obama ameapa kuhakikisha wanampata mtu aliyewatumia vijana hao wawili kama chambo ya kutekeleza mashambulizi hayo.