Thursday, May 02, 2013

KOREA KASKAZINI YAMHUKUMU RAIA WA MAREKANI

Mahakama ya Juu ya Korea Kaskazini imemhukumu raia mmoja wa Marekani miaka 15 ya kazi ngumu kwa kupatikana na hatia ya kile kilichotajwa kuwa ni "vitendo vya uhasama" dhidi ya serikali ya nchi hiyo. Kenneth Bae, mwenye umri wa miaka 44 anayewaongoza watalii, alikuwa alizuru mji wa Rason mwezi Novemba mwaka jana akiwa na watu wengine wanne. Alikuwa amezuiliwa na polisi tangu wakati huo. Hukumu hiyo imeufanya uhusiano baina ya Marekani na Korea Kaskazini kuwa mbaya zaidi. Inafuatia wiki kadhaa za vita vya maneno kufuatia hatua ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la kombora la nyuklia lililopigwa marufuku. Jumatatu Marekani ilitoa wito wa kuachiwa ria wake huyo.

IDADI YA VIFO BANGLADESH YAFIKIA 430

Waokoaji wamepata miili zaidi ndani ya vifusi vya jengo la kiwanda cha nguo lililoporomoka nchini Bangladesh, wakati maafisa wakisema huenda ikachukua siku nyingine tano kuondoa vifusi hivyo. Mbali na watu 430 waliothibitishwa kufa, polisi wameripoti kuwa wengine 149 bado hawajulikani waliko, kufuatia mkasa huo ambao ndio mbaya zaidi kuwahi kuikumba sekta ya nguo nchini Bangladesh. Miili 20 imegunduliwa usiku wa kuamkia leo huku waokoaji wakiamini kuwa miili zaidi imefunikwa katika ghorofa ya chini ya jengo hilo lililokuwa la ghorofa nane na sasa wanatumia mashine ili kuondoa vifusi hivyo. Wakati huo huo Meya wa mji wa Savar ambao mkasa huo ulitokea, Mohammed Refat Ullah, amewachishwa kazi kwa kuidhinisha kujengwa jumba hilo la Rana Plaza bila kufuata sheria. Mmiliki wa jengo hilo pamoja na babake ni miongoni mwa watu wanane wanaozuiliwa na polisi.

MPATANISHI WA MGOGORO WA SYRIA APANGA KUJIUZULU


Mpatanishi wa mgogoro wa Syria nchini ya Umoja wa Mataifa UN, Lakhdar Brahimi anatarajia kujiuzulu kufuatia kuwepo kwa mvutano miongoni mwa Jumuia ya kimataifa katika jitihada za kumaliza machafuko ya Syria. Brahimi aliyechukua nafasi ya Kiongozi wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan mwezi Agosti mwaka jana anataka kujiuzulu, hata hivyo ameshawishiwa kusubiri kwa siku kadhaa. Kama ilivyokuwa kwa Annan, Brahimi amekuwa akionesha kutofurahishwa na mgawanyiko ndani ya Umoja wa Mataifa juu ya Syria, Urusi ikiunga mkono Utawala wa Rais wa Syria, Bashar Al Assad, huku mataifa ya Magharibi na jumuia ya nchi za ghuba zikiunga mkono upinzani.
Wakati huo huo Marekani imeapa kupata ukweli juu ya shutma kuwa utawala wa Rais Assad nchini Syria unatumia Silaha za kemikali kupambana na Waasi nchini humo kabla ya kuchukua hatua zaidi. Hata hivyo hatua imepingwa vikali na serikali ya Syria kupitia kwa Balozi wa Syria ndani ya Umoja wa Mataifa, Bashaar Jafaari. Serikali ya Marekani tayari imeviagiza vyombo vyake vya usalama kuandaa hatua za kuchukua baada ya nchi hiyo kujiridhisha na ushadi kuhusu majeshi ya Syria kutumia silaha za kemikali.

MAREKANI KUTOIONDOA CUBA KATIKA NCHI ZINAZOUNGA MKONO UGAIDI


Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetangaza kwamba haina mpango wowote wa kuliondowa taifa la Cuba kwenye orodha ya nchi zinazo tuhumiwa kuunga mkono Ugaidi, kama ilivyo kwa Syria, Iran, Sudan. Naibu msemaji wa wizara Patrick Ventell amesema hakuna mpango wowote wa mabadiliko katika orodha hiyo ya nchi zinazounga mkono ugaidi, na hakuna nia ya kuiondowa Cuba katika orodha.
Wizara hiyo ya mambo ya nje ya Marekani imekuwa ikitagaza orodha kila mwaka ya nchi na mashirika yanayo unga mkono ugaidi, ripoti ambayo hutolewa kila April 30, lakini mwaka huu ripoti jhiyo imeahirishwa kutolewa na huenda ikawekwa kabla ya mwezi huu wa Mei kumalizika. Wakati huohuo Wanaharakati kutoka Jumuia ya Kimataifa wametoa wito kwa Marekani kuheshimu na kuhakikisha Wafungwa wa gereza ya guantanamo wanapata haki yao ya kuishi, huduma za afya,na haki nyingine za msingi.
Wanaharakati wametoa wito huo baada ya kuripotiwa kuwa takriban Wafungwa 100 katika Gereza hilo kwako katika mgomo wa kutokula, 21 kati yao wamekuwa wakilazimishwa kula kwa njia ya mipira ya puani. Wataalam wa maswala ya haki za binaadam wamesema wamepokea taarifa juu ya madhara ya kisaikolojia na kimwili kufuatia kuwepo kwa sintofahamu juu ya mustakabali wa maisha yao.
Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia maswala ya haki za Binaadam mjini Geneva, Rupert Colville amesema kuwa Mamlaka nchini Marekani inakiuka Wajibu wao wa kulinda haki za binaadam kimataifa.

SERIKALI YA CHAD YAZIMA NJAMA ZA MAPINDUZI

Vikosi vya usalama nchini Chad vimevunja njama ya kuipindua serikali ya Rais Idriss Deby. Duru zinaarifu kuwa njama hiyo imekuwa ikipangwa kwa muda wa miezi kadhaa. Waziri wa Mawasilian wa Chad Hassan Sylla Bakary amesoma taarifa kupitia televisheni ya taifa na kusema, ‘Mei mosi kundi la watu wenye nia mbaya walikuwa wamepanga vitendo vya kuvuruga taasisi za jamhuri.’ Amesema vikosi vya usalama nchini humo vimekuwa vikifuatilia wapanga njama hao tokea Desemba mwaka 2012.
Chad ina historia ndefu ya njama za mapinduzi na Deby mwenyewe aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1990.Tokea wakati huo ameshinda chaguzi nne na amejitangaza kuwa muitifaki mkubwa wa nchi za Magharibi katika kile kinachodaiwa ni vita dhidi ya magaidi katika eneo kubwa la Sahel barani Afrika.Bakary amesema waliopanga njama hiyo wametiwa mbaroni na kukabidhiwa vyombo vya mahakama. Hata hivyo hakubainisha utmabulisha wa waliopanga najama. Duru za kijeshi Chad zinasema maafisa kadhaa jeshini wameshatiwa mbaroni kwa kuhusika na njama hiyo.

CUBA YAITAKA MAREKANI KUIFUNGA GUANTANAMO


Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Rodriguez Parrilla ameitaka Marekani ifunge jela iliyozusha mjadala mkubwa ya Guantanamo Bay na kukirejesha kituo hicho cha kijeshi kwa serikali ya Havana.
Parilla amesema hayo katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva na kuongeza kuwa, kuna wasiwasi mkubwa kuhusu hatua za muda mrefu na za ukiukaji wa haki za binadamu zinazochokuliwa dhidi ya mahabusi wanaoshikiliwa katika jela hiyo iliyo kwenye ardhi ya Cuba iliyoghusubiwa na Marekani. Amesema, inasikitisha kuona kuwa Guantanamo Bay kimekuwa kituo cha mateso na vifo vya wanaoshikiliwa. Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba yametolewa siku moja baada ya Rais Barack Obama wa Marekani kuahidi kufanya jitihada mpya za kufunga jela hiyo ya kijeshi. Marekani inawashikilia watu 166 huko Guantanamo Bay ambao wengi wao wamekamatwa bila kujulikana makosa yao wala kufikishwa mahakamani.

WAFANYAKAZI NA SHIRIKA LA LUFTHANSA WAAFIKIANA JUU YA MISHAHARA

Shirika kubwa la ndege la Ujerumani Lufthansa na chama cha wafanyakazi cha verdi vimekubaliana nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi takriban 33,000 wa shirika hilo.Shirika la habari la Ujerumani dpa limesema leo kuwa wafanyakazi hao watapata nyongeza ya kati ya asilimia 3 na 4.7 na kuhakikishiwa kazi zao kwa kipindi cha miezi 26 ijayo.Wiki iliyopita wafanyakazi hao wa Lufthansa walishiriki katika mgomo wakidai nyongeza ya mishahara.Karibu ndege 1700 zilisitisha usafiri kutokana na mgomo huo ambao uliwawacha zaidi ya abiria 150,000 wakiwa wamekwama.Mwanzoni chama hicho cha wafanyakazi kilitaka nyongeza ya asilimia 5.2 na hakikisho la kusalia katika ajira kwa miezi 29. Lufthansa inajaribu kupunguza gharama ili kukabliana na bei ya juu ya mafuta na ushindani mkali kutoka mashirika mengine ya ndege ya Ulaya na kutoka eneo la ghuba kama Emirates,Qatar na Etihad.

JESHI LA AFGHANISTAN KUONGOZA ULINZI WAKATI NATI IKIONDOKA

Jeshi la Afghanistan litachukua jukumu la kuongoza operesheni za kusimamia usalama nchini humo katika kipindi cha miezi  miwili ijayo huku majeshi ya jumuiya ya kujihami ya Nato yakijiondowa.Msemaji wa wizara ya ulinzi Zahir Azimi amesema jeshi la nchi hiyo liko tayari kuongoza operesheni hizo.Tangazo hilo linakuja huku kundi la wanamgambo la Taliban likitangaza mwanzo wa msimu mpya wa mashambulio dhidi ya majeshi ya kigeni na ya Afghanistan pamoja na wafanyakazi wa umma.Mjini London wizara ya ulinzi ya Uingereza imethibitisha kuwa wanajeshi watatu waliouwawa hapo jana katika shambulio la bomu walikuwa raia wa Uingereza.Wanajeshi tisa kutoka Afghanistan pia walifariki katika shambulio hilo la bomu ya kutegwa kando ya barabara.Vifo hivyo vya jana vimefikisha 444 idadi ya wanajeshi wa Uingereza waliouwawa Afghanistan tangu mwaka 2011.Mapema leo wanamgambo walimuua afisa mmoja wa baraza kuu la amani Malim Shawali pamoja na mlinzi wake katika jimbo la Helmand.

MFARANSA ANAYEHUSSISHWA NA UGAIDI AKAMATWA MALI


Raia wa Ufaransa aliyeshukiwa kuwa mfuasi wa kundi la kigaidi baada ya kuonekana katika picha ya Video akiionya Ufaransa juu ya uvamizi wake nchini Mali, amekamatwa na Vikosi vya Ufaransa kaskazini mwa Mali. Chanzo cha Habari cha Serikali ya Mali kimethibitisha kimethibitisha kukamatwa kwa raia huyo wa Ufaransa . Gille le Guen ambaye anajulikana kwa jini la Abdel Jelil aliyekamatwa karibu na mji wa Timbuktu mwishoni mwa juma, atahojiwa nchini Mali kabla ya kusafirishwa kupelekwa nchini Ufaransa.

Mtu huyo anaaminika kuwa mfuasi wa Alqaeda wa AQIM baada ya yeye na Familia yake kuhamia nchini Mali akitokea nchini Morocco na Mauritania ambapo pia aliwahi kuishi. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaeleza kufanikiwa kwa jitihada za vikosi vya Ufaransa kupambana na wanamgambo wa kiislamu kaskazini mwa Mali. Umoja wa Mataifa upo mbioni kupeleka jeshi la kimataifa nchini Mali ili kuchukua nafasi ya wanajeshi ya Ufaransa ambao tayari wameshaanza kuondoka nchini humo.

IDARA YA USALAMA YA MAREKANI YAFIKIRIA HATUA DHIDI YA SYRIA


Rais wa Marekani Barack Obama amesema kuwa Serikali yake itafikiri upya juu ya hatua za kuchua ikiwa itabainika kuwa silaha za kemikali zilitumiwa na utawala wa Rais wa Syria, Bashar Al Assad. Obama amesema kuwa idara ya ulinzi na Mashirika mengine ya Usalama yameamriwa kufanya maandalizi kwa hatua yeyote itakayochukuliwa ikiwa itabainika silaha za kemikali zilitumika. Obama alizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ripoti ya kiintelijensia ya Marekani kuwa majeshi ya Syria yamekuwa yakitumia silaha za kemikali japo Marekani ilishaonya kuhusu matumizi ya silaha hizo.

Rais Obama amesema kuwa hawezi kuchukua hatua yoyote mpaka apate ukweli na kujiridhisha juu ya taarifa hiyo na endapo utawala wa Bashar Al Assad utadhihirika basi Marekani itachukua hatua kulingana na mapendekezo yaliyotolewa na vyombo vya usalama. Serikali ya Assad imekuwa ikishutumiwa kutumia silaha hizo katika maeneo ya Makazi ya Raia huku, Balozi wa Syria ndani ya Umoja wa Mataifa, Bashar Jafaari akikana shutuma hizo akisema kuwa Wapinzani nchini humo wamekuwa wakitumia silaha hizo hasa walipofanya shambulizi karibu na mji wa Idlib nchini humo. Serikali ya Syria imeikatalia timu ya wachunguzi kutoka umoja wa Mataifa kuingia nchini Syria na kuchunguza ukweli juu ya matumizi ya Silaha za kemikali katika mgogoro wa nchi hiyo ambao kwa mujibu wa Takwimu za Umoja wa Mataifa, Zaidi ya watu elfu sabini wamepoteza maisha.

ALSHABAB WAAPA KULIPIZA KISASI


Kundi la al Shabab nchini Somalia limetishia kulipiza kisasi dhidi ya viongozi wa eneo linalojitawala la Puntland lililoko kaskazini mwa Somalia, baada ya kuuawa wanamgambo 13 wa kundi hilo.
Msemaji wa al Shabab amesema kuwa, watalipiza kisasi dhidi ya viongozi wa Puntland kwa vile wamewauwa kwa halaiki wanamgambo wa kundi hilo. Ameongeza kuwa, wale wote waliohusika katika kufanya ujasusi, kutoa ushahidi wa uwongo na kuwahukumu adhabu ya kifo wanamgambo hao wa al Shabab, watakabiliwa na hatima mbaya.
Vikosi vya usalama wa Puntland vimewekwa katika hali ya tahadhari kwa shabaha ya kukabiliana na shambulio la kulipiza kisasi la kundi la al Shabab. Imeelezwa kuwa, kwa miaka kadhaa sasa eneo la Puntland limekuwa tulivu, lakini hivi sasa wanamgambo wa al Shabab wanavuruga utulivu wa eneo hilo. Viongozi wa Puntland wanasema kuwa, wanamgambo wengi wa al Shabab wamejizatiti katika maeneo ya milimani ya magharibi mwa mji wa bandari wa Bosasso.

KUENDELEA KWA MASHAMBULIZI YA ISRAEL UKANDA WA GHAZA


Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema kuwa, mashambulizi ya ndege za utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza ni hatua ya hatari na isiyokubalika. Fauzi Barhum msemaji wa Hamas amesema, lengo la mashambulizi hayo ni kulikosesha amani eneo la Gaza ili kufunika uhalifu unaotekelezwa na utawala huo katika mji wa Quds katika operesheni za kuuyahudisha mji huo, ujenzi wa vitongoji na kushtadi bila kukoma kukamatwa ovyo wakaazi wa mji huo. Barhum ameongeza kuwa, adui Mzayuni ametambua madhara na matokeo ya jinai zake hizo, na kwamba kushambuliwa Gaza ni hatua ya hatari na ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya usitishaji vita.  Hii ni katika hali ambayo, maeneo mengine ya Palestina pia yanashuhudia vitendo vya utumiaji mabavu vya Israel huku wakaazi wake wakiendelea kukandamizwa. Israel mara kadhaa imekiuka makubaliano ya usitishaji vita iliyofikia na Wapalestina kufuatia kushindwa kwake katika vita vya siku 8 dhidi ya Gaza, Novemba mwaka 2012. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Israel ilitakiwa kutofanya shambulizi lolote dhidi ya maeneo ya Palestina na kujiepusha na hatua za kuwachokoza Wapalestina. Lakini jinai dhidi ya Wapalestina zimeongezeka hasa baada ya Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel kuunda Baraza lake jipya la Mawaziri linalohesabiwa kuwa la kufurutu ada zaidi kuliko la huko nyuma. Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Marekani katika kutekeleza sera zao za kila siku za kinafiki mkabala na Wapalestina, wanataka kuonyesha kuwa Israel inakusudia kufanya jitihada mpya za kuleta amani katika eneo. Kuhusu hilo John Kerry Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani na baadhi ya waitifaki wake wa nchi za Kiarabu katika kikao kilichofanyika mjini Washington wametaka kuanza tena kwa mwenendo eti wa kusaka amani kati ya Israel na Wapalestina. Kikao hicho kilihudhiriwa pia na Joe Baiden Makamu wa Rais wa Marekani, Nabil al Arabi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Hamad bin Jassim al Thani, Waziri Mkuu wa Qatar. Katika mazungumzo hayo Kerry alitangaza kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa Marekani kazungumzia tena mpango wa amani uliopendekezwa na Saudi Arabia mwaka 2002 unaojulikana kama 'Mpango wa amani wa Kiarabu.'
Mpango huo unaeleza suala la kurejeshwa katika hali ya kawaida uhusiano wa nchi za Kiarabu na Israel sambamba na utawala huo kuondoka katika baadhi ya maeneo unayoyakalia kwa mabavu ya Palestina yaani ardhi zilizoghusubiwa mwaka 1967. Sisitizo la Marekani la kufuatilia Mpango wa Amani wa Kiarabu linatokana na kuwa, mpango huo licha ya kushinikiza Mamlaka ya Ndani ya Palestina iipe fursa zaidi Israel, unafumbia macho haki za wananchi wa Palestina ikiwemo haki ya kurejea wakimbizi wa Palestina katika nchi yao, kadhia ya mateka wa Palestina na Quds kuwa mji mkuu wa nchi huru ijayo ya Palestina. Mabadiliko yanayojiri sasa huko Palestina yanaonesha kuwa, Wapalestina wanakabiliwa na hatua zinazoshtadi za utumiaji mabavu za Israel na vilevile njama za Marekani na serikali za Kiarabu, ambazo zinafuatilia kuwa na maelewano na utawala huo haramu. Lakini tahadhari ya Wapalestina kwa utawala huo na waungaji mkono wake inaonyesha jinsi walivyokuwa macho na njama hizo. Pia inaonesha kuwa, Wapalestina kamwe hawatishwi na siasa za ukandamizaji za Israel na kama huko nyuma hawatodanganyika na madai ya upatanishi ya maadui wa taifa hilo, yaani Marekani na baadhi ya serikali za Kiarabu.

WANAFUNZI WA AL AZHAR WALISHWA CHAKULA CHENYE SUMU

Habari kutoka Cairo, mji mkuu wa Misri zinasema kuwa, zaidi ya wanafunzi 160 wa chuo kikuu cha Al-Azhar wamelazwa hospitalini wakiwa katika hali mahututi baada ya kula chakula chenye sumu. Habari zaidi zinasema Rais Mohammad Mursi wa nchi hiyo ameagiza uchunguzi ufanywe mara moja kuhusiana na tukio hilo. Wizara ya Afya ya Misri imesema sumu hiyo ilikuwa kwenye samaki wa mkebe. Tukio hilo ni la pili kutokea katika kipindi cha mwezi mmoja. Majuma kadhaa yaliyopita, zaidi ya wanafunzi 500 katika chuo kikuu hicho mashuhuri walilazwa hospitalini baada ya kula chakula chenye sumu. Jambo hilo lilipelekea wanafunzi kugoma na kuandamana na matokeo yake yakawa ni kupigwa kalamu msimamizi mkuu wa chuo hicho. Al-Azhar ni moja kati ya vyuo vikuu vinavyosifika Misri na ushawishi wake umejipenyeza hadi katika safu za juu za uongozi wa nchi hiyo.

WIZARA YA SHERIA YAZINGIRWA LIBYA

Maafisa wa Libya wamesema kuwa watu kadhaa wenye silaha wamelizingira jengo la Wizara ya Sheria ya nchi hiyo huko Tripoli mji mkuu wa Libya. Walid bin Rabha, Mkuu wa Idara ya Habari ya Wizara ya Sheria ya Libya amesema kuwa, watu kadhaa wenye bunduki za kutungulia ndege wamelizingira jengo la wizara hiyo wakiwa kwenye magari. Rabha ameongeza kuwa, watu hao wenye silaha walimtaka Waziri wa Sheria na wafanyakazi waliokuwemo ndani ya wizara hiyo kuondoka ofisini na kuifunga wizara hiyo. Tangu jana Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya nayo inazingirwa na watu wenye silaha wapatao 200. Watu hao wamezitaka wizara hizo mbili kuwazuia masalia ya wafuasi wa utawala wa Muammar Gaddafi wasishike nyadhifa muhimu na wameipa serikali ya Libya muda wa siku tatu iwe imewafukuza masalia wote wa utawala wa zamani wa nchi hiyo.

RAIS WA ZAMANI WA TUNISIA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA

Kwa mara nyingine mahakama ya kijeshi nchini Tunisia imemuhukumu dikteta wa nchi hiyo aliyekimbia nchi kifungo cha maisha jela bila ya kuwepo mahakamani. Hii ni mara ya tatu kwa mahakama hiyo ya kijeshi nchini Tunisia kumuhukumu dikteta Zainul Abidin Bin Ali kwa makosa ya mauaji dhidi ya wananchi katika harakati za mapinduzi ya wananchi za mwaka 2010 na 2011. Wakati huo huo Rafik Haj Kassem, Waziri wa Mambo ya Ndani wa utawala wa Bin Ali, amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela huku Ali Saryati, Mkuu wa zamani wa Idara ya Usalama ya Tunisia akifutiwa tuhuma zote zilizokuwa inamkabili. Inasemekana kwamba, familia ambayo ilimpoteza mtu mmoja au kujeruhiwa watu wawili wa familia hiyo katika harakati za mapinduzi hayo, italipwa kuanzia Dinar elfu 12 hadi laki moja sarafu ya Tunisia, sawa na Dola za Kimarekani elfu nane hadi elfu sabini.