Sunday, May 05, 2013

IRAN YALAANI KUHUJUMIWA KWA KABURI LA HUJR BIN ADI, SYRIA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amewaandikia barua wakuu wa taasisi kadhaa za kimataifa akilaani vikali kuvunjiwa heshima na kufukuliwa kaburi la sahaba wa Mtume SAW na Imam Ali (as), Hujr bin Adi, huko Syria. Katika barua hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Akbar Salehi mbali na kulaani kitendo cha watu wenye kufurutu mipaka ambao wamelihujumu kaburi hilo, ametaka hatua za dharura zichukuliwe kwa lengo la kuwaadhibu waliohusika na kitendo hicho kichafu. Salehi ametuma barua tatu tafauti kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO. Katika barua hiyo Salehi amelaani kitendo hicho kilicho dhidi ya ubinaadamu na kinachokiuka akhlaqi na kusema taasisi hizo za kimataifa zinapaswa kuchukua hatua kali na za kivitendo ili kurejesha heshima ya sahaba huyo wa Mtume SAW. Salehi amesema kuna haja ya kulinda maeneo matakatifu ya dini mbali mbali na kuonya kuwa kitendo kama hicho cha kuvunja kaburi la sahaba ni jambo linaloweza kuchochea mapigano ya kidini na kimadhehebu. Wakati huo huo wanazuoni wa ngazi za juu wa kidini kote Iran wamelaani vikali kitendo hicho kiovu cha kuhujumu kaburu la sahaba mkubwa wa Mtume SAW. Hali kadhalika wanafunzi wa vyuo vya kidini katika mji mtakatifu wa Qum na Tehran jana walifanya maandamano makubwa kulaani kitendo hicho cha kinyama. Siku ya Alkhamisi Mawahabi wenye misimamo ya kufurutu ada katika kundi la kigaidi Syria linalojiita ‘Jabhat An-Nusra’ walivamia na kufukua kaburi la Hujr bin Adi sahaba mkubwa wa Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW na Imam Ali (as) huko Damascus mji mkuu wa Syria.

ISRAEL YASHAMBULIA SYRIA

Israel imethibitisha kuwa ilifanya shambulio la angani dhidi ya Syria ikilenga meli iliyokuwa imebeba shehena ya silaha zinazodaiwa kupelekwa kwa kundi la wanamgambo  wa  Hezbollah nchini Lebanon usiku wa kuamkia jana.Serikali ya Marekani imesema inayumkinika kabisa kwamba Israel imefanya shambulio hilo. Shambulio hilo linashukiwa kulenga shehena ya silaha zinazodaiwa kupelekwa kwa kundi la wanamgambo wa Hezbollah, lenye makao yake katika nchi jirani ya Lebanon. Kituo cha Televisheni cha CNN  kimesema  taarifa hizo za kijasusi ni kwa mujibu wa mashirika ya kijasusi ya Marekani na mataifa ya magharibi. Afisa  mwandamizi  wa  Marekani amekiambia  kituo  cha  televisheni  cha  NBC  kuwa  mashambulio hayo  huenda  yanahusika  na  kuharibu  kituo cha  silaha  za kemikali. Maafisa  wa  Ikulu  ya  Marekani  na  wizara  ya  ulinzi wamekataa  kuzungumzia  lolote  kuhusu  ripoti  hiyo.Duru zinaarifu kuwa Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Alhamisi jioni alifanya kikao cha faragha na baraza lake la usalama mjini Jerusalem ambapo aliidhinisha shambulio hilo la angani.Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Jafar amesema hana taarifa zozote kuhusu shambulio hilo.

JAPAN KUIJENGEA UTURUKI KIWANDA CHA NYUKLIA

Japan na Uturuki zimesaini makubaliano ya ujenzi wa kinu kikubwa cha nyuklia kitakachojengwa na Japan katika pwani ya Bahari Nyeusi nchini Uturuki. Makubaliano hayo yametiwa saini mjini Ankara kati ya Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe ikiwa ni sehemu ya ziara ndefu ya Waziri Mkuu wa Japan katika Mashariki ya Kati. Waziri Mkuu wa Uturuki ameusifu mkataba huo wa ujenzi wa kiwanda cha nyuklia utakaogharimu dola bilioni 22 na kuuelezea kuwa ni "hatua muhimu sana" itakayobadilisha uhusiano kati ya nchi yake na Japan kuwa wa "ushirika wa kistratijia". Kampuni ya ubia ya Japana na Ufaransa ndio iliyoshinda kandarasi ya ujenzi wa kiwanda cha pili cha nyuklia cha Uturuki yanayoelezewa kuwa ni mafanikio ya kwanza kwa Japan katika miradi ya nyuklia nje ya nchi tangu ilipofikwa na janga la nyuklia mnamo mwezi Machi mwaka 2011 katika kinu chake cha nishati ya atomiki cha Fukushima

Saturday, May 04, 2013

MAPIGANO MAKALI YASHUHUDIWA NCHINI LIBYA


Mapigano makali yameshuhudiwa nchini Libya baada ya baadhi ya wananchi kuandamana wakipinga hatua ya wapiganaji kupiga kambi kwa takribani juma moja wakitaka kufukuzwa kazi kwa maofisa wote waliokuwa wakifanya kazi katika serikali ya Rais wa zamani wa nchi hiyo marehemu Kanali Muammar Ghaddafi. Mamia ya watu walikusanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli kupinga kitendo cha wapiganaji hao ambao wamejihami kwa silaha kuendelea kusalia nje ya majengo ya wizara ya mambo ya nje na ile ya sheria.
Hakuna taarifa za majeruhi wala kifo katika ghasia hizo ingawa kumekuwepo na taarifa za baadhi ya vikundi vya watu wenye silaha kuendelea kuwatishia waandamanaji wanaopingana nao katika miji mingine ya nchi hiyo ukiwamo ule wa mashariki wa Benghazi. Wapiganaji hao wengi wao ni wale walioshiriki mapambano yaliyofanikisha harakati za kumuondoa madarakani Kanali Ghaddafi aliyefariki dunia mnamo mwaka 2011. 
Serikali ya Libya imekuwa ikipitia pendekezo la sheria ya kuwaondoa Maofisa watu waliokuwa chini ya utawala wa Kanali Ghaddafi ambao bado wameendelea kusalia katika nyadhifa za juu.
Wachambuzi wa siasa za nchi hiyo wanaona kuwa iwapo pendekezo hilo litapitishwa na kuwa sheria litawaathiri wengi na kusababisha mifarakano na chuki kuendelea kukita mizizi katika Taifa hilo.

NCHI KADHAA ZATAKA KUBADILISHWA MUNDO WA UN

Nchi kadhaa wanachama wa Umoja wa Mataifa zimetaka ubadilishwe  muundo wa umoja huo na badala yake kuwe na haki sawa kwa wanachama wote wa umoja huo. Mwakilishi wa Uswisi katika Umoja wa Mataifa akiwa mwakilishi wa kundi la zaidi ya nchi 15 kwenye umoja huo amesema kuwa, wanachama wa Umoja wa Mataifa ambao sio wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanapasa kuwa na haki zaidi kwenye umoja huo, na kusisitiza kwamba Umoja wa Mataifa unapasa kufanyiwa marekebisho ya kimsingi, kwani nchi zote wanachama wa umoja huo zinalazimika kutelekeza maazimio ya Baraza la Usalama. Nchi za Uswisi, Ireland, Uruguay, Norway na nchi nyingine 10 zimeunda kundi linalopigania haki sawa  kwenye umoja huo hata  kwa nchi zisizo wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama.  Kundi hilo pia limeeleza kuwa, kura ya veto si ya kisheria, kwani kwa miaka kadhaa sasa Washington imekuwa ikiitumia vibaya kura ya veto kwa kuukingia kifua utawala wa Kizayuni wa Israel.

KUONDOKA WANAJESHI WA ETHIOPIA SOMALIA

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwa askari wote wa jeshi la nchi hiyo wameondoka katika ardhi ya Somalia. Wanajeshi wa Ethiopia waliingia katika ardhi ya Somalia mwezi Novemba mwaka 2011 kwa lengo la kushirikiana na wanajeshi wa Kenya pamoja na vikosi vya serikali ya mpito ya Somalia katika operesheni za kuwatomeza wanamgambo wa kundi la Ash Shabab. Kwa kuondoka kundi la mwisho la wanajeshi waliokuweko katika mji wa Baidoa huko kusini magharibi mwa Somalia, kuwepo kijeshi kwa Ethiopia ndani ya ardhi ya Somalia kumefikia tamati. Hata hivyo askari wa jeshi la Kenya ambao waliingia nchini Somalia mwezi Oktoba miaka miwili iliyopita kwa madhumuni ya kuwasaka na kuwatokomeza wanamgambo wa Ash Shabab, wao wataendelea kubakia nchini humo. Baada ya kupata idhini rasmi iliyotolewa na Umoja wa Afrika mnamo mwezi Januari mwaka huu, wanajeshi wa Kenya walijiunga rasmi na operesheni ya umoja huo ya kurejesha amani nchini Somalia AMISOM. Baada ya kuondoka wanajeshi wa Ethiopia jukumu la kulinda amani na kurejesha utulivu katika mji wa Baidoa limekabidhiwa kwa vikosi vya AMISOM.

Friday, May 03, 2013

HUKUMU YA SHEIKIH PONDA MAY 9

Kutoka AHLU SUNNAH GROUP ON FACEBOOK.


Hukumu ya Sheikh Ponda Issa Ponda (Hafidhahullah) na Waislamu wenzake 49 wiki ijayo InshaALLAH. Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar es Salaam imepanga Mei 9 mwaka huu, kuwa siku ya hukumu ya kesi ya Sheikh Ponda Issa Ponda (Hafidhahullah) na wenzake 49. Waislamu wengine 52 tayari wameshahukumiwa miaka mitatu jela. LAA HAULA WALAA KHUWATA ILAA BILAAH, Ndugu zetu wanateswa kwa ajili ya kusema Mola wetu ni ALLAH. May 9 mwaka tufike mahakamani kwa ajili ya Kusikiliza Hukumu ya Ndugu zetu InshaALLAH.

Dua Zetu Muhimu sana kwa Ndugu zetu Waislamu Popote walipo, 
ALLAH awape Subira Katika Mitihani hii ya Dunia ALLAH awazidishie Iman na Taqwa (Ucha Mungu) Amiin.

GAZETI ANNUUR MAY 3, 2013

ANNUUR 1069 by Hassan Khamis

MATOKEO YA FORM FOUR KUFUTWA


HABARI zilizotoka bungeni mjini Dodoma muda huu ni  kwamba matokeo yote ya  kidato  cha  nne 2012 yamefutwa na mitihani itasahihishwa upya haraka iwezekanavyo.
Taarifa ya tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuchunguza sababu za kufeli vibaya kwa watahiniwa wa kidato cha nne kwa mwaka jana imesomwa  leo bungeni  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Waziri Lukuvi amesema sababu zilizosababisha wanafunzi  hao kufeli ni pamoja na upungufu wa waalimu, mazingira magumu ya kufundishia, idadi kubwa ya shule za sekondari iliyopelekea idadi kubwa ya watahiniwa  na  utaratibu  mbovu  wa  Baraza  la  Mitihani Tanzania (NECTA) uliotumika  bila  kuwashirikisha  wadau mbalimbali  wa  elimu.
Kutokana na sababu hizo, matokeo yote ya kidato cha nne 2012 yamefutwa na mitihani itasahihishwa upya.

NDEGE YA JESHI LA MAREKANI YAANGUKA NA KUUA WANAJESHI


Ndege ya jeshi la Marekani imeanguka katika eneo la milima katika jimbo la Chuy nchini Kyrgyzstan. Maafisa wamesema kuwa watu watatu waliokuwa ndani ya ndege hiyo aina ya C-130, wote wanahofiwa kufariki. Ndege hiyo ilianguka muda mfupi baada ya kuruka kutoka uwanja wa jeshi la Marekani la Manas, ambao ni muhimu kwa operesheni za jeshi la nchi hiyo nchini Afghanistan.
Wizara ya Kyrgyzstan inayohusika na masuala ya dharura imesema kuwa hakuna aliyenusurika ajali hiyo, lakini taarifa za baadhi ya watu walioshuhudia ajali ya ndege hiyo zimeeleza kuwa rubani aliruka kwa kutumia mwavuli. Maafisa wa Marekani wamesema kuwa bado wanafanya uchunguzi kupata uhakika wa kile kilichotokea. Mwambata wa kijeshi wa Marekani nchini Kyrgyzstan aliripotiwa kutembelea eneo ilikotokea ajali hiyo.

MVUTANO WA KOREA MBILI WAENDELEA


Wafanyakazi wa mwisho waliobakia wa Korea Kusini katika kiwanda cha pamoja  ndani ya  Korea kaskazini wamerejea nyumbani leo. Kurudi kwao kuanakamilisha hatua ya kuondoka kwa Korea kusini katika eneo hilo, kukiwa na  hali ya wasiwasi mkubwa katika rasi ya Korea.
Msemaji wa serikali mjini Seoul alisema kulipatikana maelewano juu ya masuala ya  malipo  yaliosalia na  Korea Kaskazini na  hatimae Wakorea Kusini  kukubaliwa kuvuka mpaka kurudi nyumbani. Kurejea nyumbani kwa wafanyakazi saba  kutoka kiwanda cha Kaesong kulizuiliwa tangu Jumatatu, baada ya Korea Kaskazini kuadai malipo ya mishahara  ya nyuma pamoja na  kodi inayokadiriwa kufikia karibu dola milioni 80.
Korea Kusini iliamua kujiondoa katika eneo hilo  la kiviwanda la pamoja wiki iliopita, baada ya Korea Kaskazini kukataa wito wa mazungumzo juu ya kufunguliwa tena kiwanda cha Kaesong. Shughuli zilisisimamishwa tarehe 19 mwezi uliopita, wakati Korea Kaskazini ilipowaondoa wafanyakazi wake 53,000, kwa sababu ya  mazoezi ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini pamoja na mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

WAASI WA SYRIA WASEMA WANAPATA MAFUNZO TOKA NCHI ZA NJE

Ripoti mpya inaonyesha kuwa, Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zimekuwa zikitoa mafunzo ya kijeshi kwa makundi ya kigaidi yaliyoko Syria. Kamanda mmoja wa kundi linalojiita Free Syrian Army (FSA) amesema kuwa wapiganaji wao wamekuwa wakipata mafunzo hayo huko Jordan na wahusika wakuu ni Marekani na Ufaransa. Kamanda huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe ameiambia kanali ya BBC kwa njia ya simu kwamba, mafunzo hayo yamechukua wiki mbili na yamejikita zaidi katika matumizi ya silaha za kawaida kama vile maguruneti, mizinga na makombora ya masafa mafupi. Huku hayo yakijiri, uchunguzi wa maoni uliofanywa na shirika la habari la Reuters umebaini kuwa zaidi ya asilimia 60 ya Wamarekani hawaungi mkono nchi yao kuingilia kijeshi kadhia ya Syria. Wamarekani waliohojiwa kwenye uchunguzi huo wa maoni wamesema nchi yao inakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi na hivyo utakuwa ni uchakaramu wa kupindukia iwapo serikali itatumia fedha za umma kuingia katika vita vingine.

SYRIA YASISITIZA KUFELI NJAMA ZA ISRAEL

Naibu Waziri wa Habari wa Syria amesema kuwa, njama za Utawala wa Kizayuni dhidi ya nchi yake, zimefeli. Khalaf al-Miftah ameyasema hayo mapema leo katika mahojiano na televisheni ya Kiarabu ya Al-Alam na kusisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni unafanya njama usiku na mchana ili uweze kufanikisha malengo yake katika mgogoro unaoendelea nchini Syria lakini njama hizo zimefeli. Aidha ameitaja hotuba ya Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebabon Sayyid Hassan Nasrullah kuwa yenye umuhimu mkubwa kwa eneo na kusisitiza kuwa, Wazayuni walikuwa wakifanya njama za kuitenga Syria na muqawama lakini hotuba hiyo imethibitisha kwamba, harakati ya mapambano imejiandaa vilivyo kujibu mashambulizi yoyote na kuudhihirishia utawala huo kuwa, ulikuwa unakosea mahesabu. Kwa upande mwengine Naibu Waziri wa Habari wa Syria Khalaf al-Miftah amezungumzia uwezo mkubwa wa jeshi la Syria wa kukabiliana na kila aina ya uingiliaji wa nje wa kijeshi nchini humo na kusema kuwa, jeshi la Syria litakabiliana vikali na uingiliaji wowote wa madola ya kigeni.

WAZIRI WA MASHAURI NIGER ATAKA NGUVU ZITUMIKE KUZUIA WANAMGAMGO WA LIBYA

Waziri wa Mashauri ya Kigeni nchini Niger ametaka kutumiwa nguvu kubwa ya kijeshi ya kimataifa kwenda kupambana na watu wenye silaha huko kusini mwa Libya ambao amesema ni tishio kubwa kwa nchi za jirani. Mohamed Bazoum amesema hayo katika mazungumzo yake na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius mjini Paris na kuongeza kuwa, Niger ina taarifa za kuaminika zinazoonyesha kwamba, makundi ya wanamgambo waliofukuzwa kaskazini mwa Mali, sasa yamepiga kambi katika maeneo ya kusini mwa Libya, suala ambalo ni tishio kubwa kwa usalama wa nchi za jirani na Libya. Akiongea na waandishi wa habari, Mohamed Bazoum amesisitiza kuwa, nchi za Mali na Libya zinapaswa kupewa umuhimu wa hali ya juu zaidi. Serikali ya Libya imekuwa ikifanya juhudi za kurejesha hali ya utulivu na amani nchini humo tangu ulipong'olewa madarakani utawala a Muammar Gaddafi miaka miwili iliyopita huku ikiwa na wasiwasi kuwa wanamgambo wa kundi la al Qaida wameingia nchini humo.

SHIRIKA LA HAKI ZA BINADAMU LAITAKA UN KUZUIA MATUMIZI YA DRONE

Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch HRW, limetaka kukomeshwa matumizi ya ndege zisizo na rubani duniani. Ripoti ya shirika hilo imetaka kutolewa azimio la kukomeshwa uzalishaji, usafirishaji na utumiwaji wa ndege hizo duniani. Aidha ripoti hiyo imesisitiza kuwa, utumiwaji wa roboti za kivita au ndege zisizo na rubani umezua wasiwasi kwa kiasi kikubwa hasa kuhusiana na maisha ya watu katika kipindi cha vita. Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch pia limeongeza kuwa, utumiwaji wa ndege hizo unakinzana kikamilifu na haki za binaadamu na sheria za kimataifa na haukubaliki hata kidogo. Hii ni katika hali ambayo maelfu ya raia wasio na hatia wanauliwa kikatili kila uchao katika mashambulio ya ndege zisizo na rubani yanayofanywa na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA katika nchi mbalimbali kama vile Afghanistan, Pakistan, Yemen, Somalia na kadhalika.