Tuesday, August 07, 2012

Laylatul-Qadr- Vipi Tunaweza Kuupata Usiku Huu?

Tunaingia kumi la mwisho, kumi ambalo ndani yake kuna siku tukufu, siku ya Laylatul-Qadr, ambayo ibada yake ni bora kuliko ibada ya miezi elfu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala: ﴿


 بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ ﴾ إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ - وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ - لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ - تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ - سَلَامٌ هِيَ حَتَّى مَطْلَعِ الْفَجْرِ 
KWA JINA LA ALLAAH MWINGI WA REHMA MWENYE KUREHEMU - Hakika Sisi Tumeiteremsha Qur-aan katika Laylatul Qadr, Usiku wa Cheo Kitukufu -Na nini kitachokujuulisha nini Laylatul Qadr?- Laylatul-Qadr ni bora kuliko miezi elfu - Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao Mlezi kwa kila jambo - Amani usiku huo mpaka mapambazuko ya alfajiri. [Al-Qadr: 1-5) 

 Vile vile dalili katika Hadiyth mbali mbali zimethibiti kuhusu Fadhila za usiku huu mtukufu, na jinsi Mtume (swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa hali yake katika siku hizi kumi za mwisho za Ramadhaan. 

 Baada ya kuzijua fadhila zake usiku huu mtukufu inakupasa Muislamu ujikaze katika siku kumi hizi za mwisho kuacha mambo yote yanayokushughulisha ya dunia na utumbukie katika ibada tu ili uweze kuupata usiku huo mtukufu, yaani ukukute wewe ukiwa katika ibada ili zihesabiwe ibada zako kama kwamba umefanya ibada ya miezi elfu. 


 Tukifanya hesabu miezi elfu hiyo ni sawa na umri wa miaka 83! 1000 ÷ 12 = 83.3 yaani miaka themanini na tatu na miezi mitatu takriban. Hivyo ikiwa Laylatul-Qadr imekukuta katika ibada ya aina yoyote, ikiwa ni Swalah (Qiyaamul-Layl), kusoma Qur-aan, kufanya aina za dhikr, kutoa sadaka, kulisha chakula, kuwasiliana na jamaa, kujielimisha au kuelimisha, kufanya wema kwa watu, yote hayo utaandikiwa kama umefanya hayo kwa umri wa miaka 83! 

Na juu ya hivyo ibada hiyo ya usiku mmoja tu ni bora zaidi kuliko ibada utakayoweza kufanya miaka 83 na miezi mitatu. Subhaana Allaah! Jihadhari ndugu Muislamu usije ukakukuta usiku huu mtukufu ukiwa katika maasi au katika sehemu ukiwa umeghafilika na ya dunia kama sokoni, magenge ya soga au michezo ya kupoteza wakati au kwenye televisheni ukiangalia misalsalaat, mipira na sinema zikakupita kheri zote za usiku huu. Utaona siku hizi Waislamu wengi wanashughulika kwenda madukani kutafuta nguo za 'Iyd khaswa kina dada wakiacha masiku haya yawapite wakiwa humo badala ya kuwa majumbani mwao au misikitini kufanya ibada na kutegemea kuupata usiku huu.

 Ni siku chache tu ndugu Waislamu ambazo zinakimbia kama upepo. Je, nani basi katika sisi atakayepuuza asiupate usiku huo? Na Nani katika sisi atafanya hima kuupata usiku huo? Kwani hatujui kama tutakuweko duniani mwakani kuzipata siku hizi au hata hatujui kama tutaikamilisha Ramadhaan hii. Basi tujitahidi kwa kukesha siku kumi hizi na kuamsha familia zetu ili iwe kheri yetu kukutana na usiku huo mtukufu tuweze kupata fadhila zake hizo ambazo ni sawa na kulipwa malipo ya umri mrefu kama tulivyoona hapo nyuma hata kama hatutoruzukiwa umri huo. 

 Mwenye Kuukosa Usiku Huu Amekula Khasara Kubwa: 

 Hakika mwenye kuukosa usiku huo atakuwa amenyimwa kheri zake na itakuwa ni khasara kuukosa usiku huu mtukufu kama anavyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):


 عَنْ أَبِي هُرَيْرَة رَضِيَ اللَّه عَنْهُ قَالَ : لَمَّا حَضَرَ رَمَضَان قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ (( قَدْ جَاءَكُمْ شَهْرُ رَمَضَان شَهْرٌ مُبَارَكٌ اِفْتَرَضَ اللَّهُ عَلَيْكُمْ صِيَامَهُ تُفْتَح فِيهِ أَبْوَاب الْجَنَّة وَتُغْلَق فِيهِ أَبْوَابُ الْجَحِيم وَتُغَلُّ فِيهِ الشَّيَاطِين فِيهِ لَيْلَة خَيْرٌ مِنْ أَلْف شَهْر مَنْ حَرُمَ خَيْرهَا فَقَدْ حُرِمَ)) وَرَوَاهُ النَّسَائِيّ 

 Kutoka kwa Abu Huraryah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba ilipofika Ramadhaan, amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, ni mwezi wa Baraka. Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni Fardh, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi elfu. Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa haswa)) [An-Nasaaiy] Siku hiyo ni siku iliyoteremeshwa Qur-aan kutoka mbingu ya saba hadi mbingu ya kwanza kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala): ﴿

 بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ ﴾ حم - وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ - إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ - فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ

 KWA JINA LA ALLAAH MWINGI WA REHMA MWENYE KUREHEMU - Haa Miym - Naapa kwa Kitabu kinachobainisha - Hakika Tumekiteremsha katika usiku uliobarikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji - Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima. [Ad-Dukhaan: 1-4] Aya ya nne inayosema 'Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikma' kuwa kuna makadirio ya mwaka huo na yote yatakayotokea katika mwaka mzima. Kwa maana kwamba, siku ya Laylatul-Qadr, makadirio yote yaliyomo katika Al-Lawhum-Mahfuudhw (Ubao uliohifadhiwa) na huteremshwa haya makadirio na Malaika ambao wanaandika makadirio ya mwaka unaokuja yakiwa ni kuhusu umri wetu wa kuishi, rizki zetu, na yatakayotokea yote hadi mwisho wake.

 [Imesimuliwa na Ibn 'Umar, Mujaahid, Abu Maalik, Adh-Dhwahaak na wengineo katika Salaf – Ibn Kathiyr: 8:671] Kujikaza kufanya ibada: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa inapoingia kumi la mwisho akijikaza kwa kufanya ibada kuliko siku zozote zingine: 

 عن عائشة – رضي الله عنها- قالت: " كان رسول الله – صلى الله عليه وسلم- يجتهد 
في العشر الأواخر، ما لا يجتهد في غيره" مسلم

 Kutoka kwa mama wa waumini bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba: "Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijitahidi katika kumi la mwisho kuliko alivyojitahidi katika siku nyingine zozote" [Muslim] Na katika Swahiyhayn (Al-Bukhaariy na Muslim): 

 عن عائشة رضي الله عنها، قالت: "كان رسول الله صلى الله عليه وسلّم إذادخل العشر شذ مئزره، وأحيا ليله، وأيقظ أهله ( وفي رواية) "أحيا الليل،وأيقظ أهله، وجدّ، وشدّ المئزر" رواه البخاري ومسلم،.

 Kutoka kwake pia mama wa waumini bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha): "Ilipokuwa inaingia kumi (la mwisho) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaza izaar (shuka) yake, akikesha usiku, na akiamsha ahli zake" (Na katika riwaaya nyingine) "Akikesha usiku, akiamsha ahli zake, akijitahidi na akikaza izaar yake" [Al-Bukhaariy na Muslim] Kwa Nini Umeitwa Laylatul-Qadr? Amesema Shaykh Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu-Llaah): 
 - Kwanza: Kutokana na uwezo nao ni utukufu kama vile kusema “fulani mwenye uwezo mkubwa" yaani mwenye hadhi au utukufu. 
 - Pili: Ni usiku ambao una makadirio ya mwaka mzima na huandikwa yote yatakayotokea mwaka huo, na hii ni Hikma ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) na kuonyesha usanifu wa utengenezaji Wake na Uumbaji Wake. 
 - Tatu: Usiku huo una uwezo mkubwa kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((من قام ليلة القدر إيمانا واحتسابا غفر له ما تقدم من ذنبه)) متفق عليه ((Atakayesimama usiku wa Laylatul-Qadr kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim Sababu Ya Kupewa Waislamu Laylatul-Qadr:

 Sababu ya kupewa Ummah huu wetu wa Kiislamu siku hii tukufu ya Laylatul-Qadr ni kwamba: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliona umri wa Ummah za mwanzo ni mrefu, na umri wa Ummah wake ni mfupi akapewa usiku wa Laylatul-Qadr uwe ni bora kuliko miezi elfu. [Muwatwtwaa 1/321 (Muhammad Fuad 'Abdul-Baaqy] Ibada Za Kufanya Masiku Kumi Haya Katika Kukesha: Qiyaamul-Layl:(Kisimamo cha usiku kuswali)

 ((من قام رمضان إيماناً واحتساباً غفر له ما تقدم من ذنبه)) متفق عليه

 ((Atakayesimama (Kuswali) Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim] Kuosma Qur-aan: Khaswa kwa vile usiku wa Laylatul-Qadr ndio usiku ulioteremeshwa Qur-aan kama tulivyoona katika Aayah hizo za juu katika Suratul-Qadr na Suratud-Dukhaan. Vile vile Ramadhaan nzima inampasa Muislamu asome Qur-aan kwani ni mwezi ulioteremshwa Qur-aan kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala): 

 ((شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ))

 ((Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi)) [Al-Baqarah: 185] Na Jibriyl ('Alayhis-Salaam) alikuwa akimteremkia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila usiku wa Ramadhaan akimsomesha na kumsikiliza Qur-aan: "

كَانَ رَسُولُ اللَّهِ -صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ- أَجْوَدَ النَّاسِ وَكَانَ أَجْوَدُ مَا يَكُونُ فِي رَمَضَانَ حِينَ يَلْقَاهُ جِبْرِيلُ وَكَانَ يَلْقَاهُ فِي كُلِّ لَيْلَةٍ مِنْ رَمَضَانَ فَيُدَارِسُهُ الْقُرْآنَ" رواه البخاري

 Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, na alikuwa mbora zaidi katika Ramadhaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur-aan)) [Al-Bukhaariy] Kufanya I'tikaaf: Kutia nia kubakia msikitini kwa kufanya ibada tu humo kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya hivyo:

 عن عائشة – رضي الله عنها- قالت "كان النبي يعتكف في كل رمضان عشرة أيام؛ فلما كان العام الذي قبض فيه اعتكف عشرين يوماً - أخرجه البخاري

 Kutoka kwa mama wa waumini bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba: Mtume (swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya I'tikaaf kila Ramadhaan siku kumi, ulipofika mwaka wake wa kuaga dunia alifanya I'tikaaf siku ishirini" [Al-Bukhaariy] Kuomba Maghfirah: Kwani usipoghufuriwa madhambi yako basi ni hatari! 

 عَنْ أَنَس وَغَيْره أَنَّ النَّبِيّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لَمَّا صَعِدَ الْمِنْبَر ثُمَّ قَالَ (( آمِينَ آمِينَ آمِينَ)) " قِيلَ يَا رَسُول اللَّه عَلَامَ مَا أَمَّنْت ؟ قَالَ (( أَتَانِي جِبْرِيل فَقَالَ يَا مُحَمَّد رَغِمَ أَنْف رَجُل ذُكِرْت عِنْده فَلَمْ يُصَلِّ عَلَيْك قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ ثُمَّ قَالَ رَغِمَ أَنْف رَجُل دَخَلَ عَلَيْهِ شَهْر رَمَضَان ثُمَّ خَرَجَ فَلَمْ يُغْفَر لَهُ قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ ثُمَّ قَالَ رَغِمَ أَنْف رَجُل أَدْرَكَ وَالِدَيْهِ أَوْ أَحَدهمَا فَلَمْ يُدْخِلَاهُ الْجَنَّة قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ )) صحيح الترمذي و قال الشيخ الأباني حسن صحيح 

 Kutoka kwa Anas na wengineo kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipopanda juu ya minbar aliitikia ((Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn)). Alipoulizwa kwa nini ameitikia hivyo akasema: ((Amenijia Jibriyl akasema: Ewe Muhammad, ole wake yule ambaye unapotajwa hakuswalii, hivyo sema Aamiyn. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: ole wake yule ambaye umeingia mwezi wa Ramadhaan kisha akatoka bila ya kughufuriwa, kwa hiyo sema Aamiyn. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: 

ole wake yule ambaye amewakuta wazazi wake au mmoja wa wazazi wake lakini wasimuingize Peponi. Hivyo sema Aamiyn. Nikasema Aamiyn)) [Swahiyh At-Tirmidhiy na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa Hadiyth hiyo ina daraja ya Hasan Swahiyh] Du'aa Ya Kuomba Maghfirah Katika Siku Kumi Hizi Zakaatul-Fitwr Mwisho:

 عن عائشة رضي الله عنها أنها قالت يا رسول الله أرأيت إن وافقت ليلة القدر ما أدعو قال: ((تقولين: اَللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌ تُحِبُّ الْعَفْو فَاعْفُ عَنِّي)) ابن ماجه و صححه الألباني

 Kutoka kwa mama wa waumini bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba alisema "Ewe Mjumbe wa Allaah je, nitakapowafikiswha usiku wa Laylatul-Qadr niombe nini?" Akasema, ((Sema: Ewe Allaah Hakika Wewe Ndiye Mwenye Kusamehe Unapenda Kusamehe basi Nisamehe)) [Ibn Maajah na kaisahihisha Al-Albaaniy] Matamshi Yake: 

 Allaahumma Innaka 'Afuwwun Tuhibbul-'Afwa Fa'afu 'Anniy Kumkumbuka Allaah Kwa Aina Zozote Za Dhikr: Kwa Tasbiyh, Tahmiyd, Tahliyl, Takbiyr (kusema: Subhaana Allaah, Alhamdulillah, Laa Ilaaha Illa Allaah, Allaahu Akbar) Kuomba Du'aa: Kwa vile ni mwezi wa kuomba Du'aa pia kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala Ameunganisha Aayah za kufaridhishwa Swawm na Aaya za kuhusu kuomba Du'aa:

 ((وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُواْ لِي وَلْيُؤْمِنُواْ بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ)) 

 ((Na waja Wangu watakapokuuliza khabari Zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka)) [al-Baqarah: 186] Usiku Gani Khaswa Unapatikana Laylatul-Qadr?
 Hadiyth zimetaja siku kadhaa ambazo usiku huu mtukufu hutokea katika siku kumi za mwisho na haswa katika usiku wa witiri, zikiwa zimetajwa nyingine kuwa ni usiku wa siku ya ishirini na moja, au ishirni na tatu, au ishirni na tano au ishirini na saba kama ilivyokuja katika dalili zifuatazo:

 لحديث عائشة أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((تحروا ليلة القدر في الوتر من العشر الأواخر)) رواه البخاري 

 Hadiyth kutoka mama wa waumini bibi 'Aiashah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Utafuteni usiku wa Laylatul-Qadr katika siku za witiri kwenye siku kumi za mwisho)) [Al-Bukhaariy] 

 وفي حديث ابن عباس رضي الله عنهما أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: (( التمسوها في العشر الأواخر من رمضان ليلة القدر في تاسعة تبقى ، في سابعة تبقى ، في خامسة تبقى)) رواه البخاري 

 Hadiyth kutoka Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Utafuteni usiku wa Laylatul-Qadr katika siku kumi za mwisho za Ramadhaan, katika (usiku wa) tisa, saba, na wa tano utakaobakia [mwisho wa Ramadhaan])) [al-Bukhaariy] Imaam Ahmad amerikodi kutoka kwa 'Ubaydah bin As-Swaamit kwamba alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu usiku wa Laylatul-Qadr akasema: 

 ((فِي رَمَضَان فَالْتَمِسُوهَا فِي الْعَشْر الْأَوَاخِر فَإِنَّهَا فِي وِتْر إِحْدَى وَعِشْرِينَ أَوْ ثَلَاث وَعِشْرِينَ أَوْ خَمْس وَعِشْرِينَ أَوْ سَبْع وَعِشْرِينَ أَوْ تِسْع وَعِشْرِينَ أَوْ فِي آخِر لَيْلَة ))

 ((Katika Ramadhaan, utafuteni siku kumi za mwisho, hakika umo katika siku za witiri, siku ya ishirini na moja, au ishirini na tatu, au ishirini na tano, au ishirini na saba, au ishirini na tisa, au usiku wa mwisho)) [Ahmad] Alama Zinazobainisha Laylatul-Qadr: Kwenye usiku huo kunakuwa na mwanga zaidi. Upepo siku hiyo hutulia, yaani siku hiyo hautokei upepo mkali. Hali ya hewa huwa nzuri. Nyoyo siku hizo huwa na utulivu na unyenyekevu zaidi kuliko siku nyingine. Baadhi ya watu wema huoteshwa usiku kama walivyokuwa wakioteshwa Maswahaba na Salafus-Swaalih (wema waliotangulia) Asubuhi Yake:

 حديث أبي بن كعب رضي الله عنه أنه قال : "أخبرنا رسول الله صلى الله عليه وسلم أنها تطلع يومئذ ٍ لا شعاع لها" رواه مسلم 

 Hadiyth kutoka kwa Ubay bin Ka'ab (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba: "Ametuambia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa jua hutoka siku hiyo likiwa halina mishale (mikali)" [Muslim]

 (( ليلة القدر ليلة طلقة لا حارة ولا باردة ، تُصبح الشمس يومها حمراء ضعيفة)) صحيح ابن خزيمة 

 ((Laylatul-Qadr usiku ulio katika hali ya ukunjufu, usio na baridi wala joto, asubuhi yake jua huwa jekundu na dhaifu)) [Swahiyh Ibn Khuzaymah] 

 ليلة القدر ليلة بلجة (أي مضيئة) لا حارة ولا باردة ، لا يرمى فيها بنجم)) (أي لا ترسل فيها الشهب) رواه الطبراني ومسند أحمد 

 ((Laylatul-Qadr usiku wa kung'aa [yaani wenye mwanga] sio joto wala baridi, na vimondo (nyota za kufyatuliwa) hazitotumwa)) [At-Twabaraaniy na Ahmad] Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kukesha masiku haya kumi ili tujaaliwe kuupata usiku huu mtukufu tutoke katika Ramadhaan hii tukiwa tumeghufuriwa madhambi yetu yote na tumepewa fadhila za usiku huu mtukufu zinazolingana na kuongezewa umri wa miaka 83. Aamiyn

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO