Saturday, February 02, 2013

MALENGO YA NYUMA YA PAZIA YA W/MKUU WA UINGEREZA LIBYA


David Cameroon Waziri Mkuu wa Uingereza akishiriki kwenye mkutano wa waandishi wa habari pamoja na Ali Zidan Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Libya mjini Tripoli amesema kuwa, serikali ya London iko tayari kutumia uwezo wake wote wa kijeshi  kwa shabaha ya kutoa mafunzo kwa wanajeshi na maafisa wa vikosi vya usalama vya Libya. Cameroon amebainisha kuwa lengo kuu la serikali ya Uingereza ni kuisaidia serikali ya Libya katika kuleta amani na uthabiti kamili nchini humo. Aidha amesisitiza kwamba, London iko tayari kusaidia ujenzi mpya na kuikarabati nchi hiyo iliyoharibiwa na vita. Waziri Mkuu wa Uingereza siku ya Alhamisi aliwasili nchini Libya bila ya kutolewa taarifa za awali. Duru ya pili ya uingiliaji kati wa Uingereza nchini Libya ambayo imetimia kwa kisingizio cha kusaidia ujenzi mpya,  imefanyika kwa madhumuni ya  kupora maliasili ya nchi hiyo  na hasa mafuta na gesi. Awali Uingereza ilijitumbukiza nchini humo kwa lengo la kuuondoa madarakani utawala wa dikteta Muammar Gaddafi.
Tunaweza kusema kuwa, safari za David Cameroon Waziri Mkuu wa Uingereza na ile ya Nicolas Sarkozy Rais wa zamani wa Ufaransa, zote zimefanyika kwa malengo hayohayo. Hivi sasa Libya iko katika kipindi cha kujikarabati na weledi wa masuala  ya kisiasa wanaeleza kuwa, safari za viongozi wa Ulaya nchini humo zinafanyika kwa lengo la kutia saini mikataba ya mabilioni ya dola ya kuijenga upya nchi hiyo na hali kadhalika kupora maliasili ya nchi hiyo yakiwemo mafuta. Amma swali ambalo hadi sasa bado halijapata jibu ni hili kwamba; je, ni kwa nini nchi za Magharibi katika opersheni zao za kijeshi katika kipindi cha miezi michache tu, zililenga na kuharibu kabisa miundombinu muhimu ya Libya vikiwemo viwanda vya kusafisha mafuta bila ya sababu zozote za kimsingi? Wataalamu wa masuala ya mafuta wanasema kuwa, visima vingi vya mafuta na gesi bado havijagunduliwa nchini humo. Amma maudhui nyingine ni suala la kuporwa mapinduzi ya Libya na nchi za Magharibi, katika hali ambayo, baadhi ya  wanamapinduzi walikuwa na matumaini  ya kuuangusha utawala wa  dikteta Gaddafi  kwa usaidizi tu wa nchini za Magharibi na wala si uingiliaji wao.
Hivi sasa nchi za Ulaya zikiongozwa na Ufaransa na Uingereza zinafuatilia kwa makini mabadiliko na matukio yanayoendelea  nchini Libya sanjari na kufanya  juhudi kubwa za kuishinikiza serikali ya Tripoli ishirikiane bega kwa bega na Wamagharibi. Kwa msingi huo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa, lengo la safari za hivi karibuni za viongozi wa Uingereza na Ufaransa nchini Libya  ni kufanyika juhudi za kutaka kupora na kudhibiti utajiri wa nchi hiyo baada ya kuondoshwa utawala wa Gaddafi.  Swali la kiistratijia linaloulizwa hapa ni hili kwamba, je, Wamagharibi walikuwa  na mikakati gani kwa ajili ya wananchi wa Libya baada ya kuuangusha utawala wa Gaddafi, ghairi ya kupora maliasili na utajiri wa mafuta? Tokea wananchi wa Libya walipochukua  azma ya kuangusha utawala wa Gaddafi  na Wamagharibi nao  kujitumbukiza kwenye kadhia hiyo ,nchi hizo zimeingia kwenye awamu nyingine nayo ni kuongeza satua na ushawishi wao kwa wanamapinduzi ili ziweze kufikia malengo yao machafu. Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa, mikakati mingine ya Wamagharibi nchini Libya ni kuudhofisha kadri iwezekanavyo Umoja wa Afrika, ambapo katika kadhia ya Libya umeshuhudiwa udhaifu mkubwa wa umoja huo katika kutatua mgogoro wa nchi hiyo. Kwa kutumia harakati zinazoendelea nchini Libya, Wamagharibi wataendelea kufanya juhudi za kuushinikiza  umoja huo ufanye kazi kwa maslahi yao.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO