Sunday, February 24, 2013

vituo vipya vya nyuklia kujengwa iran


Shirika la Atomiki la Iran limetangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu imeainisha maeneo 16 ya kujengwa vituo vya nishati ya nyuklia. Katika taarifa, Shirika la Atomiki la Iran limesema vituo hivyo vitajengwa katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Kaspi, Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.
Taarifa hiyo imesema miradi hiyo ni katika mpango wa muda mrefu wa Iran wa kuimarisha uwezo wake wa kuzalisha umeme wa nyuklia kwa mujibu wa kanuni za kimataifa. Wakati huo huo Shirika la Atomiki la Iran limesema migodi mipya ya madini ya urani imegunduliwa nchini na hivyo kuimarisha uwezo wa Iran kujitegemea kikamilifu katika uzalishaji nishati ya nyuklia. Kwingineko Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran Fereydoun Abbasi amesema kizazi kipya cha mashinepewa au centrifuge 180 zimeanza kutumika katika kituo cha nyuklia cha Natanz. Akizungumza Jumamosi amesema mashinepewa hizo aina ya IR2M  zitaendelea kuongezwa katika kituo hicho ili kuwezesha urutubishaji wa urani hadi kiwango cha asilimia tano. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza mara kwa mara kuwa shughuli zake za nyuklia zinafanyika kwa malengo ya amani chini ya usimamizi wa wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO