Tuesday, March 26, 2013

FAMILIA YA GADDAFI YAPEWA HIFADHI OMAN


Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Libya Muhammad Abdulaziz amesema kuwa, baadhi ya watu wa familia ya aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi wameondoka nchini Algeria na wamepewa hifadhi nchini Oman.
Matamshi ya Abdulaziz yanatolewa katika hali ambayo, siku chache zilizopita vyombo vya habari vya Oman vilitangaza kuwa, baadhi ya watu wa familia ya Gaddafi wamepewa hifadhi nchini humo kwa sababu za kibinadamu akiwemo aliyekuwa mke wa Gaddafi. Taarifa zinasema kuwa, watu waliopewa hifadhi ni wanawake na watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 na hawataruhusiwa kujishughulisha na shughuli za kisiasa au kuzungumza na vyombo vya habari.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, baada ya mji mkuu wa Libya, Tripoli kuanguka mikononi mwa wafanyamapinduzi, Safiya mke wa Gaddafi pamoja na binti yake Ayesha, na watoto wa kiume Hannibal na Muhammad walikimbilia nchini Algeria mwezi Agosti 2011.
Watoto wengine wa kiume wa Gaddafi, Saad yuko mafichoni nchini  Niger, Mu'utassim na Khamis waliuawa kwenye mapigano,  Seiful A'rab aliuawa kwenye mashambulio ya anga ya majeshi ya Nato na Seiful Islam alitiwa mbaroni nchini Libya mwezi Novemba 2011.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO