Saturday, March 09, 2013

WAPALESTINA WALALAMIKIA UJENZI WA UKUTA KATI YAKE NA ISRAEL

Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wametekeleza kitendo cha kinyama cha kuwamiminia maji taka wananchi wa Kipalestina waliokuwa wakiandamana kulalamikia  ujenzi wa ukuta wa kibaguzi wa Kizayuni katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Wanajeshi wa Israel waliwamwagia maji taka, kuwapiga kwa virungu na kuwarushia mabomu ya kutoa machozi waandamanaji wa Kipalestina katika miji ya Bala'in, Nala'in, al Ma'aswira na Bani Swaleh. Hatua ya Wazayuni ya kuwamwagia maji taka Wapalestina na hata kuzimwagia nyumba za Kipalestina maji hayo machafu, ni kitendo kinachokinzana na misingi ya kimaadili na kibinadamu, ambacho pia kimekosolewa na mashirika mbalimbali ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu. Utawala wa Kizayuni ulianza kujenga ukuta wa kibaguzi mwaka 2002 kwa lengo la kulitenga eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi za Palestina zilizoghusubiwa na Wazayuni mwaka 1948, na hadi sasa zaidi ya asilimia 80 ya ujenzi huo imeshakamilika. Imeelezwa kuwa, ukuta huo eti wa usalama, una umbali wa kilomita 750 na urefu wa karibu mita 6. Kwa kujenga ukuta huo, utawala wa Kizayuni wa Israel unataka kupora zaidi ardhi na nyumba za Wapalestina, kwani asilimia 85 ya ukuta huo imejengwa ndani ya ardhi za Palestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Katika kulalamikia kitendo hicho cha Israel kilicho kinyume na sheria, Mahakama ya Kimataifa ya The Hague mwaka 2004 ilitoa amri ya kubomolewa sehemu ya ukuta huo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Mahakama hiyo pia iliutaka utawala huo ghasibu ulipe fidia kwa Wapalestina, kwani ujenzi wa ukuta huo uliharibu majumba, mashamba na visima vya kumwagilia maji mashambani. Hata hivyo, viongozi wa Kizayuni walipuuza na wanaendelea kupuuza amri hiyo ya mahakama ya kimataifa kwa kuendelea kujenga  ukuta huo ndani ya ardhi za Palestina na kukataa kuwalipa fidia Wapalestina. Kuna zaidi ya vitongoji 100 vya Wazayuni vinavyokaliwa na zaidi ya walowezi laki tano wa Kizayuni ndani ya ardhi za Palestina. Wananchi wa Palestina hawajanyamazia kimya kitendo hicho, kwani kila siku ya Ijumaa hufanya maandamano na kupaza sauti ya kulalamikia siasa za kujitanua utawala wa Israel katika ardhi zao. Hata kama jamii ya kimataifa inaendelea kuziba masikio yake na kukataa kusikiliza kilio cha Wapalestina, amma wananchi hao madhlumu hawajakata tamaa na wameazimia kuendelea kupigania haki zao kwa uwezo wao wote.    

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO