Saturday, April 27, 2013

EU YAIKOSOA ISRAEL KUBOMOA NYUMBA ZA WAPALESTINA


Umoja wa Ulaya umeikosoa Israel kwa kubomoa majengo kadhaa ya raia wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ikiwemo al Quds ya Mashariki na hivyo kuwafanya mamia ya Wapalestina kubaki bila ya makazi. Umoja wa Ulaya umesema umesikitishwa sana na hatua ya utawala wa Tel Aviv ya kubomoa majengo 22 katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan tarehe 23 na 24 za mwezi huu, hatua ambayo imepelekea raia wa Palestina 28 kubaki bila ya makazi miongoni mwao wakiwemo watoto 18. Ubomoaji huo wa utawala wa Kizayuni umewaathiri pia Wapalestina wengine 120 wakiwemo watoto 57. Ujumbe wa Umoja wa Ulaya uliotembelea Baitul Muqaddas na Ramallah umesema kuwa baadhi ya majengo yaliyobomolewa na Israel yalijengwa kwa ufadhili wa nchi wanachama wa umoja huo.
Nyumba na majengo mbalimbali ya Wapalestina zaidi ya 2,400 yamebomolewa katika eneo C huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Baitul Muqaddas ya Mashariki tangu mwaka 2008 na hivyo kusababisha raia wa Kipalestina zaidi ya 4,400 kuwa wakimbizi.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO