Wednesday, April 24, 2013

WAFUNGWA WA KIPALESTINA WAZIDI KUPATA TABU ISRAEL

Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel limerefusha kwa miaka miwili zaidi sheria ya kibaguzi dhidi ya Wapalestina wanaoshikiliwa katika jela za kuogofya za utawala huo. Sheria hiyo iliyopitishwa huko nyuma kwenye bunge ka Israel, inaziruhusu mahakama za Israel kuongeza muda wa kuendelea kushikiliwa jela Wapalestina bila hata kuwepo wenyewe kwenye vikao vya mahakama. Bunge la Israel lilipitisha sheria hiyo miaka miwili iliyopita na kuiwasilisha kwa Baraza la Mawaziri ili irefushwe. Makundi na wanaharakati wa kisiasa wa kutetea haki za binadamu wanaamini kuwa, utawala wa Kizayuni umerefusha muda wa kushikiliwa wafungwa wa Kipalestina ili kuzuia kufichuliwa mateso wanayofanyiwa wakati wanaposhikiliwa. Israel inaamini kuwa, utesaji ni sheria na mateso ni jambo linaloruhusiwa na mahakama za utawala huo. Kwa utaratibu huo kuteshwa wafungwa wa Palestina na Israel ni jambo linalochukua sura mpya kila uchao. Inasemekana kuwa, Israel inatumia kila njia ili kuandaa mazingira ya kuendelea kuwashikilia jela Wapalestina na kuzuia kuachiliwa kwao huru kwa visingizio tofauti. Miongoni mwa njia hizo ni kushikiliwa Wapalestina bila kosa lao kujulikana wala kuhukumiwa. Huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria zote za haki za binadamu na za kimataifa, ambapo wafungwa wa Kipalestina wamekuwa wakiendelea kushikiliwa kwa muda mrefu kwenye jela hizo bila kuhukumiwa wala kufahamika tuhuma zinazowakabili. Hii ni katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni unawafanyia kila aina ya jinai mateka wa Wapalestina. Ripoti zinaeleza kuwa, Israel inaendelea kuwapiga sindano za sumu wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa kwenye jela za utawala huo, na Wapalestina wametaka kufanywe uchunguzi wa haraka wa kimataifa juu ya suala hilo. Inasemekana kuwa, duru kadhaa za kisheria na za kitiba pia zilitahadhariaha suala la Israel kuwatumia wafungwa wa Kipalestina katika majaribio ya madawa mapya, na kusisitiza kwamba, suala hilo ni kinyume cha misingi ya kimaadili ya taaluma ya tiba. Vyombo vya habari pia huko nyuma vilifuchua ripoti ya siri iliyowasilishwa na  Kamati ya Sayansi ya Bunge la Israel kwa bunge hilo kwamba, kwa mwaka maelfu ya majaribio hatari ya dawa mpya hufanywa kwa kuwatumia mateka wa Palestina, kwa kisingizio cha uchunguzi wa kitiba kwenye jela hizo. Kushtadi hatua hizo za kimabavu za utawala wa Kizayuni dhidi ya wafungwa wa Kipalestina kunadhihirisha kilele cha ukatili huo. Hii ni katika hali ambayo, kukalia kimya jamii ya kimataifa hasa Umoja wa Mataifa jinai  hizo za Israel, kimeufanya utawala huo uendeleze hatua zake hizo dhidi ya Wapalestina hasa mateka wa Kipalestina bila woga wala wasiwasi wowote. La kusikitisha zaidi ni kuwa, licha ya utawala huo kukiuka wazi haki za Wapalestina wakiwemo wafungwa, unaungwa mkono kwa dhati na serikali za nchi za Magharibi suala linaloonyesha kwamba wanakubaliana na kuendelea hatua hizo za ukikaji haki za binadamu na misingi ya kimaadili za Israel.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO