Friday, June 28, 2013

WAPINZANI MISRI KUFANYA MAANDAMANO JUNI 30

Muungano wa wapinzani unaojulikana kwa jina la Kambi ya Wokozi wa Kitaifa nchini Misri umekosoa vikali hotuba ya Rais Muhammad Morsi wa nchi hiyo, aliyoitoa jana kwa mnasaba wa sherehe za kukumbuka mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani. Wapinzani hao wamesisitiza juu ya kufanyika maandamano makubwa tarehe 30 mwezi huu dhidi ya rais huyo. Mbali na mrengo huo kusisitizia kufanya maandamano hayo ya siku ya Jumapili ijayo, pia umetaka kufanyika uchaguzi wa rais wa kabla ya wakati wake. Msemaji wa kambi hiyo Bwana Khalid Daud amekosoa tuhuma zilizotolewa na Rais Morsi na kusema kuwa hazina ushahidi wowote na kuongeza kuwa, ombi la rais huyo kwa mahakama ya katiba na kuitaka kufanya uchunguzi wa haraka wa sheria za uchaguzi wa bunge, kwa hakika ni uingiliaji wa wazi wa kiongozi huyo katika mambo ya mahakama. Daud ameongeza kuwa, viongozi wa kambi hiyo nao watashiriki katika maandamano ya tarehe 30 mwezi huu. Wakati huo huo jumuiya ya Waislamu wa madhehebu ya Kishia nchini Misri, imelaani vikali mauaji ya kikatili yaliyofanywa na Masalafi wenye misimamo mikali dhidi ya mwanazuoni maarufu wa Kishia Sheikh Hassan Shehata na wafuasi wake wengine wanne nchini Misri. Viongozi wa jumuiya hiyo waliyasema hayo hapo jana mjini Cairo mbele ya waandishi wa habari na kusema kuwa serikali iliyoshindwa kuwalinda raia wake hususan wafuasi wa madhehebu ya Kishia. Hii ni katika hali ambayo, kiongozi mmoja wa Kisalafi ametangaza hivi karibuni kuwa, mauaji hayo dhidi ya Waislamu hayo wa Kishia yalifanywa kwa idhini ya Rais Muhammad Morsi mwenyewe.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO