Friday, July 26, 2013

WAASI DARFUR WASHAMBULIA WANAJESHI

Waasi kutoka jimbo la Darfur nchini Sudan, wameshambulia kambi ya jeshi Kaskazini mwa Kordofan, na kuwaua wanajeshi 5 katika makabiliano makali . Hii ni kwa mujibu wa jeshi la nchi hiyo. Eneo la Kordofan Kaskazini halijakuwa likishuhudia mashambulizi kutokana na vurugu katika jimbo la Darfur karibu na mpaka na Sudan Kusini. Sudan Kusini imekana madai kuwa inaunga mkono waasi wa Darfur. Maelezo zaidi kuhusu mapigano hayo bado hayako wazi, ingawa makabiliano haya yanakuja kabla ya makataa ya kusitisha usafirishaji wa mafuta kutoka Sudan Kusini kutokana na madai ya kuunga waasi mkono.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011, chini ya mkataba wa mwaka 2005 wa kukomesha mapigano yaliyodumu kwa muda mrefu zaidi barani Afrika. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, uhusiano kati ya majirani hao wawili umezorota kuhusu mapato ya mafuta na tuhuma kuwa pande zote zinaunga mkono waasi kupiga mwingine. Waasi waliopigana vita vya Sudan Kusini wakati wa mapigano, walijipata upande wa mpaka wa Sudan baada ya nchi hiyo kujitenga na kisha wakachukua silaha kupigana wakidai kuwa maslahi yao bado hayatimizwi. Pamoja na makundi matatu ya waasi katika jimbo la Darfur, waliungana na kubuni kikundi cha waasi cha Sudan Revolutionary Front na wamekuwa wakiendesha harakati zao katika maeneo ya Kordofan ya Kusini na Blue Nile, ambayo yanapakana na Sudan Kusini.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO