Sunday, December 02, 2012

M23 WASHAMALIZA KUHAMA TOKA GOMA


Waasi wa M23 wameondoka kikamilifu katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Waasi hao ambao inadaiwa wanapata himaya ya Rwanda na Uganda waliuteka mji huo tarehe 20 mwezi uliopita wa Novemba. Goma ni mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini na mji huo unakadiriwa kuwa na wakaazi milioni moja. Siku ya Jumamosi wapiganaji 300 walionekana wakiondoka Goma wakiwa katika msafara wa magari waliyopora. Siku ya Ijumaa waasi hao pia waliondoka katika mji wa Sake ulio kilomita 30 magharibi mwa Goma. Brigedia Jeffrey Muheesi wa Uganda ambaye yuko katika ujumbe wa Nchi za Maziwa Makuu unaosimamia zoezi la kuondoka waasi hao Goma amesema wapiganaji wote wa M23 wameondoka mjini humo.


 Kamanda wa  M23 Brigedia Jenerali Sultani Makenga amesema wanataka serikali ya Kinshasa ianzishe mazungumzo katika muda wa masaa 48 na ameonya kuwa wanaweza kurudi tena Goma kwa mtutu wa bunduki iwapo mazungumzo yatafeli.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO