Sunday, December 02, 2012

MAUAJI YA GHAZA YAWAAMSHE WAISLAM

Kiongozi Muadhamu wa Jamhuri ya Kiislamu amesisitiza kuwa, ukatili wa Wazayuni katika mashambulizi ya watu wasio na hatia wala ulinzi wa Ghaza, yanapaswa kuamsha dhamiri ya ulimwengu wa Kiislamu na kuipa roho mpya harakati adhimu ya mataifa ya Kiislamu. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo katika mkusanyiko wa mamia ya mabasiji wa nchi nzima. Ameongeza kuwa, jinai na unyama wa Wazayuni huko Ghaza, unaonyesha ukatili uliochupa mipaka na usiofikirika wa viongozi wa utawala huo na kwamba nchi za Kiislamu hasa serikali za nchi za Kiarabu zinapaswa kubadilisha misimamo yao na kuwasaidia wananchi madhulumu lakini mashujaa wa Ukanda wa Ghaza, katika jitihada zao  za kuvunja kuzingirwa eneo hilo.


Ayatullah Khamenei aidha amesema, jinai za Wazayuni huko Gaza pia zinadhihirisha vyema sura halisi ya maadui wa Uislamu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kukosoa uungaji mkono wa viongozi wa madola ya kibeberu kwa jinai za Wazayuni amesema, Marekani, Uingereza na Ufaransa si tu hazijaukosoa hata kidogo utawala katili wa Kizayuni bali hata zinaunga mkono jinai zinazofanywa na utawala huo ghasibu, jambo ambalo linaonesha kwamba maadui wana chuki kubwa mno na umma wa Kiislamu na jinsi watawala wa madola hayo ya kibeberu walivyo mbali na maadili na ubinadamu.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO