UTAWALA WA KIZAYUNI: MADAKTARI WAENDELEA NA MGOMO
Wafanyakazi wa vituo vya afya katika
utawala wa Kizayuni wa Israel wameendelea na mgomo wao kufuatia hatua ya
utawala huo ya kupuuza matakwa yao. Wafanyakazi hao wa vituo vya afya na
wauguzi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, walifanya mgomo hapo
siku ya Jumatatu kwa siku ya nane mfululizo katika kulalamikia hatua ya utawala
huo ya kutowaongezea mishahara sambamba na kufumbia macho hali yao mbaya ya
kimaisha. Aidha wafanyakazi hao wamesistiza kuwa, mgomo huo utaendelea.
Wauguzi
pia wamesema kuwa, pamoja na maafikiano yaliyofikiwa kati yao na Wizara ya
Fedha ya Utawala haramu wa Kizayuni katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita,
kuhusiana na nyongeza ya mishahara na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi, wizara
hiyo haikutekeleza ahadi zake hatua iliyowafanya waendelee na mgomo. Kwa mujibu
wa ripoti hiyo, mgomo huo umeathiri pakubwa shughuli za baadhi ya mahospitali
na vituo vya afya vya utawala wa Israel.
Mgomo huo wa wafanyakazi wa vituo vya
afya na wauguzi unaendelea katika hali ambayo, Wizara ya Fedha ya utawala huo
ilikuwa imetishia kuwa, kama mazungumzo kati yake na Muungano wa Wauguzi
hayatafikia mwafaka na wauguzi kuendelea kugoma, itawasilisha kadhia hiyo
mahakamani kwa ajili ya kuwarejesha kazini kwa nguvu wauguzi wanaogoma. Duru
mpya ya mazungumzo kati ya Wizara ya Fedha ya Utawala Haramu wa Kizayuni na
Muungano wa Vyama vya Wauguzi, unatazamiwa kufanyika leo Jumatano.
Ikiwa ni
katika juhudi za kupunguza nakisi ya bajeti na kuokoa uchumi unaoelekea
kuporomoka wa utawala wa Israel, Baraza la Mawaziri chini ya uongozi wa
Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala huo, limeanza kutekeleza siasa za
kubana matumizi jambo ambalo limekabiliwa na upinzani mkali wa raia wa utawala
huo.
Katika hali hiyo, Mkuu wa Muungano wa Wauguzi wa Israel amenukuliwa
akisema kuwa, sekta ya uuguzi ya utawala huo inakabiliwa na mgogoro mkubwa
kufuatia idadi kubwa ya wauguzi kupungua katika miaka ya hivi karibuni na hivyo
kuathiri shughuli za afya katika mahospitali mbalimbali. Hivi sasa vituo vya
afya vya Tel Aviv, vinakabiliwa na upungufu wa wauguzi wapatao 2400, ambapo
wauguzi 400 huongezeka kila mwaka katika idadi hiyo. Matatizo ya kiuchumi na
migomo mbalimbali katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, inajiri
wakati ambao polisi ya Israel imetoa ripoti rasmi kuhusiana na ongezeko la
uhalifu na jinai katika utawala huo. Ufisadi wa kimaadili, kifedha na kiidara
kati ya watawala wa kijeshi na kisiasa wa Israel, ni matatizo mengine
yanayoukabili utawala huo, jambo ambalo limepelekea kuzuka upinzani mkubwa kati
ya Wazayuni.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO