Wednesday, January 16, 2013

JUMUIYA YA NCHI ZA KIARABU YATAKA KUUNDWA PALESTINA HURU

Nabil al-Arabi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesisitiza kwamba, amani ya kweli haiwezi kupatikana katika Mashariki ya Kati pasina ya kuundwa nchi huru ya Palestina. Nabil al-Arabi amesema hayo baada ya kumalizika kwa kikao cha pamoja cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na wenzao wa Umoja wa Ulaya na kusema kuwa, kadhia ya Palestina ndio iliyokuwa ajenda kuu ya kikao hicho na kwamba, pande mbili zimesisitiza juu ya kutatuliwa haraka hitilafu baina ya Palestina na Israel. Mbali na kadhia ya Palestina, kikao hicho kilijadili pia masuala mengine tofauti kama mahusiano ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Jamii ya kimataifa imetangaza mara kadhaa wa kadhaa kwamba, maeneo ya Palestina yaliyokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967 yanapaswa kuondoka katika makucha ya wavamizi wa Kizayuni na kwamba, madhali jeshi la Israel lingaliko katika maeneo hayo na nchi huru ya Palestina haijaundwa, basi Mashariki ya Kati, katu haiwezi kunusisha harufu ya amani na utulivu. Imepita miaka 20 sasa tangu yalipoanza mazungumzo yanayojulikana kwa jina la mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati, huku kukiwa hakuna ahadi yoyote ile ya Marekani inayojifanya mpatanishi na mbunifu wa mazungumzo hayo ambayo imetekelezwa; na mazungumzo hayo yameendelea kubakia bila natija. Mwezi Novemba mwaka 1991 Marekani iliwaita kwa mara ya kwanza katika meza ya mazungumzo Wapalestina na jamii ya Waarabu kwa ahadi ya kutekeleza maazimio mawili ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Mazungumzo hayo yalikuwa ya kwanza tangu kukaliwa kwa mabavu Palestina. Kwa mujibu wa vipengee vya maazimio hayo, jeshi la Israel linapaswa kuondoka bila masharti yoyote katika ardhi inazozikalia kwa mabavu tangu mwaka 1967 na ardhi hizo kurejeshewa wamiliki wa asili na hivyo kuandaa uwanja wa kuundwa nchi ya Palestina. Aidha inaelezwa katika vipengee vya mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati kuwa, nchi ya Palestina mji mkuu wake ukiwa Baytul Muqaddas inapaswa kuundwa mwaka 1999 baada ya kuondoka jeshi la Israel kuondoka ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Gaza na sehemu ya Baytul Muqaddas. Hata hivyo hadi leo sio tu kwamba, jeshi la Israel halijaondoka katika ardhi za Wapalestina, bali Tel Aviv hata imeongeza kasi katika kujenga na kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni hali ambayo imeondoa fursa ya kubakia ardhi kwa ajili ya kuundwa nchi ya Palestina baada ya kupita miaka 65 ya uvamizi, ukimbikizi na kubakia bila nyumba wananchi wa Palestina. Upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa ni mlolongo wa mzingiro dhidi ya ardhi za Palestina ambao umekuwa na mbinyo kiasi kwamba, ardhi za Palestina zimegawanywa na kuwa vipande vipande. Ni miongo 6 sasa ambapo eneo la Mashariki ya Kati limekuwa likishuhudia vita na machafuko huku chimbuko la hayo yote ukiwa ni uvamizi na siasa za kupenda kujitanua za utawala wa kimabavu wa Israel. Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana Nabil al-Arabi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu akasema kuwa, ili kulifanya eneo la Mashariki ya Kati lipate amani na utulivu wa kweli kuna haja ya kuandaliwa mikakati mipya ya mazungumzo na lengo la mazungumzo hayo liwe ni kuhitimishwa uvamizi wa Israel.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO