Wananchi wa Tunisia wameandamana wakiitaka serikali ya nchi hiyo kukabiliana vilivyo na umaskini na ukosefu wa ajira. Maandamano hayo yamefanyika wakati Watunisia wakijiandaa kuadhimisha mwaka wa pili tangu baada ya mapinduzi yaliyoung'oa madarakani utawala wa kidikteta nchini humo. Waandamanaji katika jimbo la Qasrina huko magharibi mwa Tunisia waliikosoa serikali kwa kutotekeleza ahadi zake. Mapinduzi ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa kidikteta wa Zainul Abidin bin Ali yalikuwa cheche ya kwanza ya mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu ambao uliziondoa madarakani tawala kadhaa za kiimla.
Wachambuzi wa mambo wanaitaja Tunisia kuwa ni kigezo bora cha mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa sasa katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika. Hata hivyo katika miezi ya mwishoni mwa mwaka 2012 na mwanzoni mwaka huu nchi hiyo ilikumbwa na maandamano yanayopinga serikali katika baadhi ya maeneo hususan katika mkoa wa Siliyaniya. Sababu kuu ya maandamano hayo ni matatizo ya kiuchumi yanayuisumbua nchi hiyo. Tunaweza kusema kuwa tatizo kuu la Tunisia na nchi nyingine za Kiarabu zilizofanya mapinduzi dhidi ya tawala za kidikteta na kiimla ni hali mbaya ya masuala ya kiuchumi na kimaisha. Baadhi ya matatizo hayo yanarejea katika kipindi cha utawala wa dikteta Zainul Abidin bin Ali na matatizo mengine yanatokana na ukosefu wa utulivu nchini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Ustawi wa uchumi wa Tunisia mwaka 2011 ulikuwa baina ya 0 na asilimia moja. Kiwango cha ukosefu wa ajira nchini humo kimeongezeka kwa asilimia 5. Sekta ya utalii ambayo katika kipindi cha utawala wa Bin Ali ilikuwa ikiingiza asilimia 8.6 ya pato ghafi la ndani na kutayarisha ajira kwa watu laki tatu na nusu, imefanya vibaya kutokana na matukio ya mwaka 2011 na taathira zake katika soko la nchi hiyo.
Wakati huo huo matukio ya Libya ambayo ni mshirika wa kwanza mkubwa wa kibiashara wa Kiarabu na Kiafrika wa Tunisia, yamekuwa na taathira nyingi mbaya kwa uchumi wa nchi hiyo. Hi ni kwa sababu karibu Watunisia elfu 40 waliokuwa wakifanya kazi nchini Libya walilazimika kurudi nchini kwao, suala ambalo limezidisha idadi ya watu wasiokuwa na ajira nchini humo. Si hayo tu bali mgogoro wa kiuchumi uliozikumba nchi za Ulaya pia umeathiri uchumi wa Tunisia kwani sehemu kubwa ya pato la nchi hiyo lilikuwa likitokana na watalii wa Kimagharibi ambao sasa wamepunguza safari zao katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kutokana na matatizo yao ya kiuchumi. Alaa kullihal, matukio ya miezi ya mwishoni mwa mwaka uliopita nchini Tunisia yameonesha kuwa, iwapo serikali ya muda ya Hamadi al Jabali haitaweza kukabiliana vilivyo na changamoto za kiuchumi hususan hali ya kimaisha ya wananchi, kutashuhudiwa malalamiko na maandamano zaidi ya wananchi dhidi ya serikali.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO