Wednesday, March 13, 2013

MAKAMANDA WA VIKOSI VYA MAJINI WA IRAN NA IRAQ WAKUTANA KUIMARISHA USALAMA ENEO LA GHUBA YA UAJEMI


Kamanda wa Vikosi vya Majini vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGG) amekutana na Kamanda wa Vikosi vya Majini wa Iraq mjini Baghdad, na kusisitiza udharura wa kuimarishwa usalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi na nchi za kieneo. Admeri Ali Fadawi alisema jana Jumanne alipokutana na Luteni Jenerali Ali Hussein Ali kuwa, uwezo wa kujilinda wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unadhamini ulinzi na usalama wa eneo hili na kwamba, haikubaliki nchi za kigeni kuwepo katika eneo hili nyeti la Ghuba ya Uajemi lenye kudhamini nishati ya dunia. Admeri Fadawi amesema, fursa imepatikana ya kuimarishwa usalama wa jumla wa nchi za eneo hili na kwamba uhusiano na ushirikiano mzuri wa Iran na Iraq unaweza kutumika kuleta amani na utulivu.  Kamanda wa Vikosi vya Majini wa Iraq naye pia alisema kuwa ushirikiano wa nchi yake na Iran una umuhimu mkubwa katika kuimarisha usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi.  
Jamhuri ya Kiislamu na Iraq kwa kuwa nchi mbili jirani na zenye uhusiano mzuri, zina nafasi muhimu katika matukio ya kieneo hasa katika kuimarisha amani ya Ghuba ya Uajemi. Hivi sasa uwezo wa kijeshi na wa kujilinda wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni wa kiwango cha juu. Suhula za kisasa za kijeshi na uwezo wa kujilinda wa vikosi vya Iran vya anga, nchi kavu na majini, umeweza kuonekana katika mazoezi tofauti ya kijeshi yaliyofanywa katika maji ya Ghuba ya Uajemi. Manuva ya vikosi vya jeshi la Iran siku zote yamekuwa yakibeba ujumbe wa amani na urafiki kwa nchi za eneo hili. Mazoezi hayo ya vikosi vya Iran nchi kavu na baharini yanaonyesha kuwa, nchi za eneo hili zina uwezo wa kuimarisha usalama wa eneo zima kwa kutegemea uwezo wao wenyewe, bila kuwepo wageni. Tajriba imethibitisha kuwa, kuwepo wanajeshi wa kigeni ndio sababu kuu ya kukosekana usalama kwenye eneo. Madhara ya kukaliwa kwa mabavu Iraq kwa karibu miaka 9 na pia Afghanistan na Marekani pamoja na vikosi vya Jumuiya ya Kujihami ya Magharibi (NATO, yanadhihirisha wazi nafasi haribifu ya vikosi vya kigeni kwenye eneo hili. Kuwepo askari wa Marekani nchini Iraq sio tu hakujahitimisha ugaidi na ukosefu wa usalama nchini humo, bali kumesababisha kuenea zaidi ugaidi, ukosefu wa amani na utulivu katika nchi hiyo. Licha ya kuwa makundi ya kigaidi kwa kuungwa mkono na Marekani na nchi za Kiarabu zilizoko pambizoni mwa Ghuba ya Uajemi, yanavuruga usalama wa Iraq, lakini serikali ya Baghdad inafanya jitihada za kurejesha usalama katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Kwa kuzingatia uwezo wa kijeshi na kisiasa wa Iraq, pamoja na ushirikiano wake na Iran katika uwanja huo, nchi hiyo inaweza kusimamia upangaji mikakati ya usalama wa jumla wa kieneo. Pia kwa kuzingatia nafasi muhimu ya Iraq katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), ambapo hivi sasa nchi hizo ni wenyekiti wa kiduru wa taasisi hizo, zinaweza kuratibu mikakati ya jumla ya kiusalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Nchi wanachama wa Arab League na NAM kila moja ina uwezo maalumu na kwa ajili hiyo iwapo zitakusanya pamoja uwezo huo, zinaweza kupata mafanikio makubwa. Kuimarishwa usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi na lango la Hormoz kunakopita zaidi ya asilimia 50 ya nishati ya dunia, kuna udharura mkubwa katika kulinda nishati hiyo. Kwa msingi huo, nchi za eneo hili hasa Iran na Iraq pamoja na Oman zina nafasi muhimu katika kufanikisha suala hilo kwa kuimarisha zaidi ushirikiano wao. 

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO