Hillary
Clinton Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani amesema kuwa, serikali ya
Washington inaitambua rasmi serikali ya Somalia. Clinton ameyasema hayo akiwa
pamoja na Rais Hassan Sheikh Mahmoud wa Somalia mbele ya waandishi wa habari
mjini Washington. Sheikh Mahmoud alijipatia ushindi kwenye uchaguzi mkuu
uliofanyika mwaka 2012, na kupata fursa ya kuiongoza nchi hiyo iliyokumbwa na
machafuko. Somalia iliyoko katika eneo la Pembe ya Afrika inahesabiwa kuwa nchi
iliyoko katika eneo nyeti na la kiistratijia. Nchi hiyo ilianza
kutumbukia kwenye machafuko na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baada ya
kuanguka utawala wa Jenerali Muhammad Siad Barre, dikteta wa zamani wa Somalia
mwaka 1991. Miaka miwili baada ya kuangushwa utawala wa Jenerali Siad Barre,
uhusiano wa Marekani na Somalia ulivunjika baada ya helkopta mbili za Marekani
kuangushwa nchini humo. Kundi la al Shabab liliweza kudhibiti eneo kubwa la
nchi hiyo wakati wa kukosekana serikali kuu nchini. Amma mwaka 2011, kundi la
al Shabab lilipoteza udhibiti wake katika maeneo mengi nchini humo, baada ya
kukabiliwa na mashambulio makali ya majeshi ya serikali ya Somalia
yakishirikiana na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika.
Kulegalega na kurejea nyuma kundi la al Shabab kuliandaa mazingira ya
kupatikana uthabiti kwa kiasi fulani, kuundwa katiba mpya, kuitishwa uchaguzi
huru wa rais na hatimaye kuteuliwa Waziri Mkuu aliyeunda serikali mpya nchini
humo. Serikali ya Somalia iliyoingia madarakani mwaka 2012, ilipongezwa na
kukaribishwa na jamii ya kimataifa. Hali ya machafuko na ukosefu wa amani
nchini Somalia na eneo zima la Pembe ya Afrika iliwatia hofu Wamarekani na
waitifaki wake wa eneo la Mashariki ya Kati na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hakuna shaka kuwa, meli za kibiashara na kijeshi za Israel zilikuwa na wasiwasi
kupita katika eneo la lango la Bab Mandab lililoko katika eneo la Pembe ya
Afrika. Ukosefu wa amani nchini Somalia, uliligeuza eneo hilo kuwa mgogoro wa
kimataifa baada ya kujitokeza vitendo vya uharamia nchini humo. Kwenye
mazungumzo na Rais Sheikh Mahmoud wa Somalia, Clinton amesema kuwa, Washington
na Mogadishu zimefungua ukurasa mpya wa uhusiano wao na kusisitiza kuwa, Washington
itakuwa mshirika kindakindaki wa Mogadishu. Naye Rais Barack Obama wa Marekani
ameahidi kuwa nchi yake itashirikiana na Somalia katika kunyanyua kiwango cha
usalama na amani, utunzaji wa fedha na kuandaa mazingira ya kutolewa huduma za
kijamii nchini humo. Mashirikiano ya pande mbili yataweza kufanikiwa kwanza kwa
kutambuliwa rasmi nchi hiyo, jambo ambalo tayari limeshatamkwa wazi na Waziri
wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani mbele ya Rais wa Somalia mjini Washington.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO