Mbunge
mmoja nchini Uingereza amekosoa vikali kukosekana demokrasia nchini humo
akihoji kwa kusema kwa nini wananchi wa nchi hiyo hawana haki ya kutoa maoni
yao kuhusu mtu wa kurithi kiti cha Malkia Elizabeth na ametaka kufanyike kura
ya maoni kuhusu suala hilo. Paul Flynn kutoka chama cha Leba amesisitiza kuwa,
ni jambo la dharura kuitishwa kura ya maoni ya kuamua iwapo mkuu wa serikali ya
Uingereza yaani Waziri Mkuu, ambaye anachaguliwa na wananchi, anawajibika
kumfuata Malkia au la, pamoja na kufanyia marekebisho sheria za mrithi wa
Malkia wa ufalme wa Uingereza. Kwa mujibu wa Katiba iliyodumu kwa muda mrefu
nchini Uingereza ni kuwa, Malkia ni cheo cha juu zaidi rasmi nchini humo licha
ya kwamba hachaguliwi kidemokrasia na ana majukumu mengi ya kidiplomasia na ya
rasmi kama vile kuidhinisha Waziri Mkuu. Malkia wa Uingereza aidha ndiye
Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya Ulinzi vya nchi hiyo licha ya kwamba
wananchi hawana nafasi yoyote ya kutoa maoni yao kuhusu nani awe Malkia na nani
arithi kiti chake. Kumekuwa na malalamiko mengi ndani ya Uingereza kuhusu
ufujaji mkubwa wa mali unaofanywa na familia ya kifalme ya nchi hiyo.
Malalamiko hayo yaliongezeka sana baada ya mwana mfalme William kufanya sherehe
ya harusi iliyojaa ufakhari na anasa kubwa kwa kufuja fedha za walipa kodi wa
Uingereza. Mirengo inayopinga kuendelea mfumo wa kifalme nchini Uingereza
imeitisha maandamano ya wananchi wakati wa sherehe za miaka 60 ya utawala wa
mfululizo wa Malkia wa hivi sasa wa Uingereza. Mirengo hiyo inataka wananchi wa
Uingereza wawe na nguvu ya mwisho wa kuamua watawaliwe na nani na kwa msingi wa
katiba gani. Naye Graham-Smith, mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya kiraia
inayopinga mfumo wa kifalme nchini Uingereza inayojulikana kwa jina la
"Jamhuri" amesema kuwa, tofauti na propaganda kubwa zinazofanywa na
vyombo vya habari vya Uingereza ambavyo kisingi vinadhibitiwa na familia ya
kifalme, wananchi walio wengi wa Uingereza hawapendi kuendelea kutawaliwa na
mfumo ambao hauwapi haki ya kuchagua viongozi wake. Naye Dk. Adrian Thurston,
mkuu wa jumuiya ya wasomi ya "Lyceum" ya mjini London amelalamikia
vikali jinsi serikali ya Uingeza inavyofuja mamilioni ya fedha za umma kwa
ajili ya kudhamini maisha ya anasa na yaliyojaa starehe ya watu wa familia ya
kifalme. Hata hivyo vyombo vya habari vya Uingereza vinajaribu kuficha
kikamilifu mitazamo ya wananchi wa nchi hiyo kuhusu Malkia na mara zote
vinaonesha kuwa wananchi wa Uingereza wanampenda kupindukia Malkia wa nchi
hiyo. Hata hivyo weledi wa mambo wanaamini kuwa si jambo rahisi hata kidogo
kukubaliwa pendekezo la kuitishwa kura ya maoni huko Uingereza kwani viongozi
walioko madarakani wanajua vyema kuwa iwapo kura hiyo ya maoni itaitishwa, basi
wananchi wataukataa bila kusita mfumo wa kifalme ambao hauwapi haki ya
kuchagua. Aidha weledi hao wa mambo wanahoji wakisema, vipi nchi kama Uingereza
inazishinikiza nchi nyingine bali hata kuzivamia kijeshi baadhi ya nchi hizo
kwa madai ya kueneza demokrasia wakati Malkia wa Uingereza yuko madarakani kwa
zaidi ya nusu karne sasa tena bila ya kuchaguliwa hata kwa kura moja ya wananchi
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO