Saturday, January 19, 2013

WAGENI NCHINI ALGERIA WATEKWA

Inaaminika kuwa wanamgambo wa Algeria wa kundi la 'Mulathameen' au 'Wenye Nikabu" wanaendelea kuwashikilia mateka raia wa kigeni katika kiwanda cha gesi maeneo ya jangwani, hata baada ya vikosi vya serikali kufanya operesheni ya kujaribu kuwakomboa. Duru za usalama za Algeria zimeripoti kuwa, katika operesheni hiyo mateka wasiopungua 30 wameuawa pamoja na wanamgambo 11 wa kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida. Miongoni mwa waliouawa ni Waalgeria 11 na raia 7 wa kigeni wakiwemo Waingereza wawili, Wajapani wawili na Mfaransa. Serikali ya Japan imelilaumu jeshi la Algeria kwa kutumia nguvu kuwakomboa mateka hao. Serikali ya Algiers imesema kuwa, imelazimika kufanya operesheni ya kijeshi kwa sababu wanamgambo walitishia kulipua kiwanda hicho cha gesi. Wanamgambo hao wamesema kuwa, wamewateka nyara raia wa kigeni ili kuitia adabu serikali ya Algeria kwa kuruhusu anga yake itumiwe na vikosi vya Ufaransa katika mashambulizi dhidi ya waasi wa Mali.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO