Wednesday, February 13, 2013

CHINA YAIONYA MAREKANI JUU YA SIASA ZAKE

Serikali ya China imeonya kwamba, vikwazo vya hivi karibuni vya Marekani dhidi ya mashirika na raia wake kadhaa kwa tuhuma za kufanya biashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vitaathiri uhusiano wa Peking na Washington. Ripoti iliyotolewa na Hung Lee, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China imeeleza kuwa, hatua hizo za Marekani zinaharibu mahusiano ya kimataifa sambamba na kuathiri maslahi ya China. Aidha ripoti hiyo imeitaka Marekani, kurekebisha mienendo yake mibaya haraka iwezekanavyo na kuondoa vikwazo hivyo dhidi ya mashirika na raia wa China ili kuepuka kutiwa doa mahusiano ya pande mbili. Itakumbukwa kuwa, siku ya Jumatatu iliyopita, Marekani ilimuwekea vikwazo mfanyabiashara mmoja wa China na mashirika kadhaa kwa tuhuma za kutotekeleza vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Marekani na waitifaki wake wameiwekea vikwazo nchi hii ikiwa ni katika jitihada mpya za Washington za kutaka kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu isimamishe shughuli zake za nyuklia zenye malengo ya amani.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO