Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Uislamu
ni dini ya ulimwengu na kwa ajili ya wanadamu wote, kwani hakuna mpaka wowote
kwenye utu na ubinadamu. Akizungumza kwenye kikao cha 12 cha wakuu wa Jumuiya ya
Ushirikiano wa OIC mjini Cairo Misri, Rais Ahmadinejad ameongeza kuwa, leo hii
ulimwengu na hasa eneo la Mashariki ya Kati linapita katika kipindi hatari mno
cha kihistoria na kusisitiza kuwa, kuna haja ya kuwekwa mikakati ya kukabiliana
na changamoto zilizopo. Akisisitizia suala la kuwepo umoja na mshikamano katika
ulimwengu wa Kiislamu, Rais Ahmadinejad ameongeza kuwa, umoja ni jambo lenye
udharura kwa serikali na wananchi. Rais wa Iran amebainisha kuwa, umasikini,
ubaguzi, udhalilishaji katika uhusiano wa kimataifa, ukandamizaji, uporaji wa
maliasili na utajiri wa mataifa huru ni miongoni mwa changamoto za pamoja
zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu.
Rais Ahmadinejad amesema kuwa, sehemu kubwa
ya matatizo ya mwanadamu yanatokana na ukandamizaji, uingiliaji kati na uadui wa
wakoloni, na kusisitiza kwamba popote duniani inapokuwepo dhulma, ubaguzi na
umasikini, bila shaka nchi za Magharibi huchangia kwa kiasi kikubwa hali hiyo,
kwani madola hayo hayatosheki hata kidogo na satua zao na kwamba lengo lao kuu
ni kudhibiti maliasili na utajiri wote ulioko ulimwenguni. Rais wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran amesema kuwa, inasikitisha kuona kwamba leo hii baadhi ya
mataifa ya Kiislamu yanacheza katika uwanja wa maadui na kushabikia migogoro na
hitilafu za ndani zilizoko baina ya wananchi na mataifa ya Kiislamu. Rais
Ahmadinejad amesisitiza kuwa madola hayo ya Kiislamu yanayocheza kwenye uwanja
wa maadui yanapaswa kuondoka katika uwanja huo; na kutumia mshikamano na uwezo
waliopewa wananchi wao ambao ni dhihirisho la nguvu za Mwenyezi Mungu, ili
kuzima fursa za mashambulizi ya maadui.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO