Naibu Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Brigedia Jenerali Mehdi Farahi amesema kuwa Tehran imefanyia majaribio - kwa mafanikio, kombora lake jipya la anga kwa anga lililotengenezwa na wanasayansi wa Iran, linalojulikana kwa jina la Fakour 90. Farahi ambaye pia ni mkurugenzi wa Taasisi ya Ulinzi wa Anga ya wizara hiyo hiyo amesema kuwa kombora hilo limefanyiwa majaribio katika ndege ya kivita ya F14. Brigedia Jenerali Farahi pia amesema, makombora mengine ya anga yanayojulikana kwa majina ya Qader yaani uwezo na Nasr yaani ushindi nayo yatafanyiwa majaribio hivi karibuni na wataalamu wa Iran. Kwenye miaka ya hivi karibuni Iran imepiga hatua kubwa katika masuala ya ulinzi na inaendelea vizuri na kampeni yake ya kujitosheleza kwa zana na vifaa vyote vya kijeshi. Iran imekuwa ikitengeneza yenyewe pia makombora mengi ya masafa tofauti na hata katika kutuma satalaiti zake anga za juu, imekuwa ikitumia makombora yake yenyewe. Farahi amesema, leo hii kuna nchi 48 zenye satalaiti anga za juu, lakini ni nchi 24 tu ndizo zenye uwezo wa kutengeneza satalaiti na ni nchi nane tu ndizo zenye zana zao zenyewe za kutuma satalaiti hizo na Iran ni miongoni mwa nchi hizo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO